April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wanawake katika sekta ya madini watakiwa kupaza sauti, kuondoa changamoto zinazowakabili

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Wanawake wanaojishughulisha katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini nchini wametakiwa kuwa na sauti ya kuweza kujisemea wenyewe ili kuondokana na kizingiti kinachokwamisha wao kujiendeleza katika shughuli ya uchimbaji waadini wanavyokutana navyo wanawake.

Meneja Mradi na Utafiti wa Taasisi ya Kuendeleza Uchimbaji Mdogo(FADev),Evans Rubara, amezungumza hayo wakati akizungumza na Timesmajira online jijini Mwanza.

Rubara ameeleza kuwa,kikubwa kinachohitajika ni wanawake kuwa na sauti na kuweza kujisemea wenyewe kwani kinachosababisha wanawake waonekane kuwa ni wachache katika sekta hiyo ni kwa vile hawawezi kujisemea.

Wanawake siyo wachache katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ila kinachosababisha waonekane wachache ni kuwa wanawake hawawezi kujisemea licha ya kuwepo kwa vyama vya wanawake wachimbaji wa madini.

Mila na desturi hususani katika maeneo hayo ya uchimbaji mdogo mfano kama Kanda ya Ziwa yani wanawake hawapaswi kusema kitu chochote ambayo hii ni changamoto kubwa sana kwani wanaona mwanamke hawezi kuruhusiwa kwenda kwenye maduara kuchimba madini.

“Wanawake wanapaswa kusikiliza na kufanya vile wanavyoambiwa,mila zetu na desturi hazimpi nafasi mwanamke za kufanya shughuli zake za kujipanua wigo kiuchumi mfano huko Mererani Arusha,kuna mwanamke mmoja ilimlazimu kujivika nguo aonekane kama mwanaume ili aingie machimboni kuchimba madini ya Tanzanite,”ameeleza Rubara.

Pia mila na desturi bado zinamuweka mwanamke kama mtu wa chini zaidi ambapo hawapati nafasi za kwenda kujifunza.

“Bado mwanamke hapewi nafasi inayostahili ili apate uwezo na kipato kwa maana ya mtaji ili aweze kufanya shughuli hizo ambapo anayefahamika ni mwenye mtaji kuliko yule anayefanya kazi kila siku,”ameeleza Rubara.

Rubara ameeleza kuwa kitu kingine ambacho kimekuwa kizingiti kikubwa kwa wanawake kujiendeleza katika sekta ya uchimbaji mdogo wa madini ni kutopata nafasi ya kujiendeleza kielimu.

Uchimbaji mdogo wa madini wa sasa unahitaji akili ule wa zamani umeisha,unakuta katika semina mbalimbali wanawake hawapati nafasi ya kuhudhuria mfano juzi mkoani Shinyanga tulikuwa na semina kikundi ambacho kilipaswa kuwa na wanawake hawakuleta mwanamke hata mmoja waliokuja ni wale vijana waoingia maduarani kuchimba,ila hawakuleta wapembuaji ambao ndio wanawake.

Aidha mbali na hayo changamoto nyingine ambayo inayofanya wanawake kukosa fursa ni uwepo wa sera ambazo haziwasaidi wanawake hivyo wanaomba iwepo sheria ambayo inawabeba wanawake na siyo sheria inayojumuisha wanawake na wanaume huku ikiwabeba wanaume zaidi.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa FADev, Mhandisi Theonestina Mwasha, ameeleza kuwa tangu enzi mwanaume ndio amekuwa akishughulika kutafuta madini na kuyatumia pia wanunuzi walikuwa wanaume.

Kwaio historia imekuwa ikiendeleza kitu hicho kuwa wanaume ndio wenye nguvu ya kwenda migodini na kufanya kazi ya uchimbaji hali hiyo ikachangia mwanamke kutojishughulisha wakidhani ni kazi ambayo mwanaume pekee ndiye anaweza kumudu.

Pia mila na desturi ambazo zimeisha wajengea wanawake kuwa kuna kazi fulani wanatakiwa kufanya na nyingine hawapaswi kufanya zimekuwa kikwazo kwa mwanamke kufanya shughuli za uchimbaji madini.

“Hali hiyo imewapelekea wao kutoweza kuthubutu kwani tukichukulia hii mikiki ya kupingwa na kutosaidiwa maana wakati mwingine hawasaidiwi kwa kuambiwa kuwa si mnaweza basi vitu vyote mfanye wenyewe,hivyo wanakata tamaa katika uchimbaji,”ameeleza Mhandisi Mwasha.

Changamoto nyingine ni jamii haijazoea kuona wanawake wanafanya shughuli za uchimbaji wa madini hivyo haiwaungi mkono hata pale wanapohitaji msaada hali hiyo inawafanya wanawake kusema hapana kazi ya uchimbaji madini tuwaachie wanaume na wao wafanye kazi nyingine ikiwemo kupika katika maeneo ya uchimbaji wa madini.