May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Jafo atilia mkazo ajenda ya Rais Dkt. Samia

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)
Dkt. Selemeni Jafo, amesema ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuanzisha kampeni ya kuhamasisha nishati safi Afrika inapaswa kuungwa mkono na watu wote, kwani takwimu zinaonesha watu milioni 4 barani Afrika wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na matumzii ya nishati chafu ikiwemo ya kuni na mkaa.

Amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa nchini yanasababisha hekta
takriban 46,242 kupotea kila mwaka kwa kukatwa kwa ajili ya kupata
kuni na mkaa.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi mitungi ya gesi 1,500 yakiwa na majiko yake kwa wananchi wa Jiji la Arusha mwishoni mwa wiki, Dkt. Jafo alisema hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Rais Samia katika kampeni ya kuhamasisha nishati safi.

“Rais Samia amekuwa na dhamira njema na ndio maana amekuja na kampeni ya nishati safi ya kupikia.Haya ni mapenzi yake na kwa sababu tunafahamu nishati chafu inamadhara makubwa
katika mazingira.

“Kwanza watu wanalazimika kutegemea kuni na mkaa kwa hiyo kuna
uharibifu wa mazingira.

Takwimu zinaonesha kila mwaka hekta 4,6242 zinapotea kwasababu ya kuni na mkaa,”alisema Dkt. Jafo.

Pia alisema takwimu zinaonesha kuwa wakinamama na wasichana kwa
asilimia kubwa wanatumia wastani wa saa 20 kwa wiki kwa ajili ya
kutafuta kuni na mkaa au wakati mwingine ni kinyesi cha wanyama.

“Leo hii ukiona nchi imejipanga katika nishati safi ya kupia ni jambo la msingi lenye kutia matumani.Watafiti wanatuambia kitendo cha kutumia nishati safi ya kupikia kwa akina mama wajazito kunasaidia kurekebisha presha ya mama mjazito,”alisema.

Aliongeza pia nishati safi inasaidia mama mjazito kupata mtoto
mwenye uzito unaokubalika anapozaliwa , hivyo kuna faida nyingi
kutumia nishati safi ya kupikia.

“Nina fahamu mpaka leo hii Oryx wameshatoa mitungi ya gesi 32,000
kwa ajili ya jamii na wameshatumia Sh.bilioni 2.7 lakini bado
wameendelea kuendelea na kampeni hiyo kwa kutoa mitungi kwa jamii.
Ameongeza kuwa Oryx wamekuwa mfano mzuri kuifikia jamii huku
akifafanua tayari Serikali imeshatoa maelekezo kwa taasisi zinazoanzia watu 100 kufunga mfumo wa kutumia nishati safi ya kupikia na tayari taasisia na mashirika ya umma yameanza kutumia nishati hiyo.

Kwa upande wake Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo amesema
katika kuunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia kuhamasisha nishati safi ya kupikia wameona ni vema kuendelea kuyagusa makundi mbalimbali katika jimbo hilo.

Alisema kuwa kabla ya kugawa mitungi hiyo 1,500 ya Oryx kwa wana
Arusha Mjini, tayari ameshagawa pia mitungi 1400 kwa wajasiriamali
huku akisisitiza wataendelea na kuyafikia makundi yote yakiwemo ya
watoto wanaolelewa vituo vya ya watoto yatima.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya gesi ya Oryx Bw.
Benoite Araman amesema madhara yanayotokana na kutumia kuni na
mkaa ani makubwa na kuwa wananchi 33,000 wanapoteza maisha kila
mwaka kwa kuvuta moshi na chembe chembe zinazotokana na mkaa na
kuni, hivyo kupikia gesi itatatua jambo hili.

Amesema kupika kwa kutumia gesi huchochea kutokukatwa kwa miti
kwa ajili ya kuni na mkaa hivyo, husaidia kulinda mazingira na wakati huo huwafanya wanawake wasitumie muda mwingi kutafuta kuni na msituni hatua itakayosaidia maandalizi ya chakula kwa wakati.

“Oryx Gas Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kutekeleza maono ya Rais kuhusu upatikanaji wa nishati. Namshukuru Mbunge wa Arusha Mjini Gambo na Serikali ya Tanzania kwa kutuunga mkono katika mipango yetu ya nishati safi kwa kuhakikisha matumizi ya gesi ya Oryx hapa Arusha na Tanzania kwa ujumla,” alisema Araman.

Wakitoa shukrani zao Wajasiriamal, Asha Mtumwa na Karim
Abdallah walieleza kuwa hatua hiyo ya kukabidhiwa mitungi ya gesi
inakwenda kuwaondolea adha waliyokuwa wakiipata kwa muda mrefu.
Wamesisitiza kuwa inaenda kuondoa athari ambazo zimekuwa
zikijitokeza kwa matumizi ya kuni na mkaa ambapo inaathari kuanzia kwenye afya pamoja na mazingira sanjari na kuokoa gharama za mkaa ambazo ni kubwa zaidi.