Na Mwandishi Wetu, Unguja
Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Ali Mwinyi ametembelea Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwenye Tamasha la Kizimkazi 2026 linalofanyika Kizimkazi, Zanzibar na kujionea namna linavyochochea uchumi wa kidigitali
Rais Mwinyi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
alipata fursa ya kufahamishwa kuhusu mchango wa Shirika katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuchochea uchumi wa kidijitali nchini.
Katika ziara hiyo Dkt. Mwinyi alipokelewa na Meneja wa TTCL Zanzibar, Nasra Mugheiry, ambaye alimweleza kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya mawasiliano inayolenga kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora, uhakika na kasi.
Akitoa maelezo kwa Rais Dkt Mwinyi Mugheiry, amemweleza Rais kuwa TTCL imeendelea kusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hatua inayowezesha upatikanaji wa miundombinu imara ya mawasiliano na kuweka msingi wa upatikanaji wa huduma mbalimbali za kidijitali.

“Mkongo huo ni sehemu muhimu ya miundombinu inayowezesha huduma za intaneti na mawasiliano kwa wananchi, taasisi za Serikali na sekta binafsi,” amesema Mugheiry
Ameeleza kuwa uwekezaji huo umeleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi, hususan kupitia huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) inayowawezesha wananchi kupata intaneti ya kasi majumbani kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya faiba.
Amesema Huduma hiyo inatoa fursa kwa familia, wanafunzi, wafanyabiashara na wataalamu kutumia intaneti kwa kujifunza, kufanya biashara, kufanya kazi kwa njia ya mtandao na kupata huduma mbalimbali za kidijitali.
Ameingeza kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni sehemu ya juhudi za Shirika katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini.
Amesema kupitia Mkongo wa Taifa na huduma za FTTH
TTCL inalenga kuwafikisha Watanzania kwenye huduma za mawasiliano za kisasa, ikiwemo intaneti ya kasi majumbani na ofisini.
Akielezea Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (National Internet Data Centre – NIDC
Mugheiry amesema kimewezeshaTaasisi za Umma, sekta binafsi na wafanyabiashara kutumia miundombinu salama ya TEHAMA.
” NIDC inatoa huduma za kisasa ikiwemo Cloud Computing, Colocation na Virtual Server, ambazo zinasaidia taasisi na biashara kuhifadhi, kuendesha na kusimamia mifumo na taarifa zao za kidijitali bila kulazimika kubeba gharama kubwa za kujenga na kuendesha miundombinu yote ya TEHAMA kwa wenyewe,” amesema
Mugheiry
Ameongeza kupitia huduma ya Cloud Computing, taasisi na biashara zinaweza kupata rasilimali za kiteknolojia kulingana na mahitaji yao, huku huduma ya Virtual Server ikiwawezesha wateja kutumia mazingira ya seva yaliyojengwa kwa teknolojia ya virtualization ndani ya miundombinu ya kituo cha data cha TTCL.
Aidha, ameongeza kuwa huduma ya Colocation inawawezesha waendeshaji wa mitandao, watangazaji na taasisi kubwa kutumia miundombinu ya TTCL kwa ajili ya kuweka vifaa vyao katika mazingira yenye huduma za umeme, ubaridi na usalama, hivyo kupunguza hitaji la kuwekeza katika miundombinu hiyo wenyewe.
Ameongeza kuwa Mkongo wa Taifa wa mawasiliano, umeongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi kupitia FTTH na kutoa miundombinu ya kuhifadhi na kuendesha huduma za kidijitali kupitia NIDC na kuwawezesha wananchi, Serikali na sekta binafsi kutumia teknolojia kama nyenzo ya maendeleo.
Ziara ya Rais Dkt. Mwinyi katika Banda la TTCL imefanyika katika kipindi ambacho Tamasha la Kizimkazi 2026 linaendelea kutoa jukwaa la kuunganisha na kufungua fursa mbalimbali. Tamasha hili kwa TTCL limekuwa fursa ya kuonesha namna teknolojia na mawasiliano inavyoweza kuunga mkono shughuli za kiuchumi na kijamii.

More Stories
MNH-Mloganzila kufanya kambi ya upandikizaji figo na urekebishaji wa mishipa ya kuchuja damu
Rais Samia asifu juhudi za Nishati Safi ya Kupikia
Gereza kwamngumi lamkabidhi aliyekuwa mfungwa vifaa vya ujenzi