September 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Matongo Mara kupata fidia

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

Wananchi hao ambao ni wakazi wa vitongoji vya Nyamilama na Masangula mkoani humo walisema hayo leo, kwamba tathmini hiyo ni hatua muhimu katika kuhakikisha ardhi, nyumba, miti na mali nyingine zinazoweza kuathiriwa na shughuli za mgodi zinatambuliwa na kupewa thamani inayostahili kabla ya maeneo yao kupisha shughuli za mradi.

Mkazi wa Kitongoji cha Nyamilama, Pius Ijukaine, amesema zoezi hilo linaendelea vizuri na kusisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na wahusika ili mchakato huo ukamilike kwa amani na kwa kuzingatia maslahi ya pande zote.

“Nimefikiwa na hili zoezi la tathmini ili kupisha maeneo ya shughuli za mgodi, hivyo naomba lifanyike kwa usahihi,” amesema.

Ijukaine amesema yeye ni mmiliki wa eneo lenye miti ya mikaratusi ambayo ni sehemu ya mali yake, hivyo anatarajia thamani ya miti hiyo kuzingatiwa wakati wa tathmini na mchakato wa fidia.

Aidha, alimeomba Barrick North Mara kuangalia uwezekano wa kuwapatia maeneo mengine wananchi ambao watapaswa kuondoka au kupisha maeneo yao kwa ajili ya shughuli za mgodi.

“Natoa wito kwa wananchi kuwa tayari ili kuepuka matatizo na kushirikiana katika zoezi hili,” amesema.

Alisema katika shamba lake amekuwa akijihusisha na kilimo cha miti aina ya mikaratusi, ambayo ni sehemu ya shughuli zake za uzalishaji na mali yenye thamani kwa familia yake.

Kwa upande wake, Elias Daniel, mkazi wa Kitongoji cha Nyamilama, amesisitiza umuhimu wa fidia kutolewa kwa usahihi kwa wananchi wenye ardhi na mali zinazoweza kuathiriwa na shughuli za mgodi.

Daniel amesema anamiliki ardhi yenye miti ya mikaratusi pamoja na miembe, hivyo aliomba mali hizo zitambuliwe na kuthaminiwa ipasavyo katika mchakato wa tathmini.

“Tunaomba fidia ziwe nzuri ili tusije kusumbua mgodi. Mimi namiliki ardhi yenye miti ya mikaratusi na miembe,”amesema.

Amesema wananchi wamekuwa wakitegemea ardhi zao kwa shughuli mbalimbali za kilimo na uzalishaji, hivyo fidia inayotolewa inapaswa kuzingatia thamani ya mali hizo pamoja na athari zinazoweza kujitokeza baada ya kupisha maeneo yao.

Naye Zubeida Saidi, mkazi wa Kitongoji cha Masangula, amesema wananchi wanahitaji uhakika kwamba mchakato wa malipo ya fidia utasimamiwa vizuri na kwa kuzingatia stahiki za kila mwananchi anayehusika.

“Naomba mgodi utupatie pesa itakayokidhi thamani ya maeneo niliyowapatia,” amesema.

Saidi amesema ni muhimu wananchi kupewa taarifa sahihi kuhusu hatua zinazofuata katika mchakato huo, ikiwemo namna thamani ya ardhi na mali nyingine itakavyobainishwa na utaratibu wa malipo ya fidia.

Amesema wananchi wanahitaji kuona mchakato huo ukienda kwa uwazi ili kila mmoja aweze kuelewa namna mali zake zilivyothaminiwa na kiasi cha fidia anachotarajiwa kupata.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nyamilama, Wambura Chacha, amesema wananchi wanatarajia kupata fidia itakayolingana na thamani halisi ya maeneo na mali zao.

Chacha amesema ushirikishwaji wa wananchi katika hatua mbalimbali za mchakato ni muhimu ili kujenga uelewa na kuondoa malalamiko yanayoweza kujitokeza wakati wa zoezi hilo.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuheshimu tamko la Serikali la kutokuendelea na ujenzi au shughuli zinazohusiana na mradi katika maeneo husika wakati mchakato wa tathmini na hatua nyingine ukiendelea.

Amesema wananchi wanapaswa kuwa watulivu na kushirikiana na viongozi pamoja na wataalamu wanaohusika ili zoezi hilo lifanyike kwa utaratibu na kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.

Kwa mujibu wa wananchi hao, matarajio yao makubwa ni kuona tathmini ya mali zao ikifanyika kwa usahihi, uwazi na kuzingatia thamani ya ardhi, miti na mali nyingine wanazomiliki.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha wananchi watakaopisha maeneo yao wanapata fidia inayolingana na stahiki zao na kuwawezesha kuanza maisha katika maeneo mengine kwa utulivu.

Aidha, wananchi walieleza kuwa mawasiliano ya mara kwa mara kati yao, viongozi na wahusika wa mchakato ni muhimu katika kuhakikisha changamoto zinazoweza kujitokeza zinatatuliwa mapema.

Wamesema ushirikiano huo unaweza kusaidia kupunguza sintofahamu na kuhakikisha zoezi la tathmini linaendelea bila migogoro, huku haki na maslahi ya wananchi yakizingatiwa.

Kwa upande wao, wananchi wamendelea kutoa wito kwa wahusika kuhakikisha kila mali inayohusika inafanyiwa tathmini kwa kuzingatia thamani yake, ili mchakato wa fidia uwe na uelewa unaokubalika kwa pande zinazohusika.