November 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaweka mikakati kutekeleza ajenda ya sifuri Tatu

Na Penina Malundo,TimesMajira

SERIKALI imeweka mikakati mitatu ya kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Sifuri Tatu ya mwaka 2026 hadi 2030, inayolenga kutokomeza uzazi wa nyumbani, vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto pamoja na watoto kukosa chanjo zinazostahili.

Mikakati hiyo inalenga kuimarisha mifumo ya afya nchini na kuhakikisha wanawake na watoto wanapata huduma bora, salama na kwa wakati, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto barani Afrika.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, amesema mkakati wa kwanza ni kuimarisha uongozi wa kisiasa, ushirikiano na uwajibikaji ili kuhakikisha afya ya mama na mtoto inakuwa kipaumbele katika maamuzi ya viongozi na mipango ya maendeleo ya taifa.

Amesema mkakati wa pili ni kuhamasisha na kuoanisha uwekezaji na mifumo ya utoaji huduma za afya, ili kuhakikisha rasilimali za ndani zinaelekezwa katika maeneo ya kipaumbele yenye matokeo chanya katika kuboresha afya ya mama na mtoto.

Ameutaja mkakati wa tatu kuwa ni kuharakisha utekelezaji wa afua zenye ushahidi wa kuokoa maisha kwa kuimarisha huduma za afya ya msingi, hatua itakayosaidia kuboresha upatikanaji na ubora wa huduma kwa wanawake na watoto.

Mchengerwa ameyasema hayo Novemba 24, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, kuhusu mikakati ya Serikali katika kutekeleza ajenda hiyo iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan nchini Ethiopia.

Amesisitiza kuwa mikakati hiyo inalenga kuhakikisha Ajenda ya Sifuri Tatu inatekelezwa kwa vitendo kupitia kuimarisha mifumo ya afya na kuweka kipaumbele katika hatua zinazochangia kuokoa maisha ya mama na mtoto.

Akifafanua malengo ya ajenda hiyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, amesema lengo la kwanza ni kutokomeza uzazi wa nyumbani kwa kuhakikisha wajawazito wanajifungulia katika vituo vya afya chini ya uangalizi wa wataalamu.

Amesema lengo la pili ni kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto wakati wa kujifungua, huku lengo la tatu likiwa ni kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa kupata chanjo zinazostahili kwa mujibu wa ratiba ya kitaifa ya chanjo.

Machumu amesema mpango huo ulizinduliwa na Rais Samia kupitia Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Afya ya Umma Barani Afrika (CPHIA 2026), unaohusisha nchi 55 za Umoja wa Afrika, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto katika bara hilo.