November 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanzania,Uganda kuimarisha Biashara na Utalii Ziwa Victoria

Na Penina Malundo,TimesMajira

KUIMARIKA kwa usafiri wa majini katika Ziwa Victoria kunatarajiwa kuchochea biashara na utalii baina ya Tanzania na Uganda, pamoja na kuimarisha muunganiko wa kibiashara kati ya maeneo ya pwani na nchi hizo mbili.

Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema Tanzania na Uganda zimekubaliana kuimarisha miundombinu ya usafiri wa reli na majini ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kukuza biashara baina ya nchi hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Novemba 24, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam, Prof.Mbarawa amesema makubaliano hayo yanalenga kuboresha muunganiko wa reli na usafiri wa majini, hatua itakayorahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupitia Reli ya Kati hadi maeneo mbalimbali ya nchi jirani, ikiwemo Uganda.

Amesema kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutasaidia kuongeza uwezo wa usafirishaji, kupunguza gharama na muda wa kusafirisha mizigo, huku kukiimarisha ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia nchi za ukanda huo.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo utafungua fursa za kiuchumi kwa vijana na wananchi wanaoishi katika maeneo yatakayopitiwa na shughuli za usafirishaji, zikiwemo huduma za bandari, upakiaji na upakuaji wa mizigo pamoja na shughuli nyingine za kibiashara.

Katika hatua nyingine, Prof.Mbarawa amesema Tanzania inalenga kuufanya Mkoa wa Tanga kuwa kitovu cha shughuli za nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki kupitia uwekezaji katika miundombinu ya mafuta, viwanda na huduma za usafirishaji.

Amesema mpango huo utahusisha uendelezaji wa miundombinu ya kupokea, kuhifadhi na kusafirisha mafuta pamoja na uzalishaji wa bidhaa zinazotokana na mafuta, zikiwemo mbolea, plastiki na kemikali.

Amesema Tanzania haitaki kubaki kuwa eneo la kupitisha mafuta pekee, bali inataka kuwa kitovu cha shughuli za kiuchumi zinazohusiana na nishati, viwanda na biashara.

“Watanzania huu ni wigo wa fursa muhimu,” amesema na kuongeza kuwa utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kufungua nafasi za ajira kwa wataalamu wa ujenzi, wahandisi, waendeshaji wa mitambo na watoa huduma za usafirishaji na ugavi.

Aidha, amesema vijana watapata fursa za kujiajiri na kujipatia kipato kupitia huduma mbalimbali zitakazohitajika wakati wa ujenzi na uendeshaji wa miundombinu hiyo.

Kuhusu Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Profesa Mbarawa amesema utekelezaji wake umefikia asilimia 93.9, huku Serikali ikiendelea kufuatilia na kusimamia kazi zilizobaki ili mradi huo ukamilike na kuanza shughuli za usafirishaji wa mafuta.