
Na Mwandishi Wetu, TimesmajiraOnline, Mbeya
VIKUNDI 39 vilivyokidhi vigezo vya kupata mikopo ya asilimia 10 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya vimeanza kupatiwa elimu ya matumizi bora ya fedha, uendeshaji wa biashara na urejeshaji wa mikopo kwa wakati.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo mwishoni mwa wiki ,Msimamizi wa Huduma za Mikopo katika Halmashauri hiyo ambaye pia ni Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Cuthbert Mwinuka, amesema katika robo hiyo halmashauri imetoa mikopo yenye thamani ya Sh941 milioni kwa vikundi hivyo.
Amesema vikundi vilivyonufaika vimeomba mikopo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo ufugaji, kilimo, ununuzi wa mazao na uendeshaji wa maduka ya pembejeo za kilimo.
Mwinuka amesema mwitikio wa wananchi kuomba mikopo hiyo umekuwa mkubwa, lakini vikundi 39 pekee ndivyo vilivyokidhi vigezo vilivyowekwa.
“Wananchi wengi wamehamasika kuomba mikopo kwa sababu idadi ya maombi ilikuwa kubwa. Hata hivyo, vikundi hivi vimeonyesha kuwa na uwezo wa kutumia mikopo hiyo. Kwa wale ambao hawakufanikiwa, tumewaandikia barua ili waboreshe maandiko yao na shughuli wanazofanya, waweze kunufaika katika robo inayofuata,” amesema.
Kuhusu athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Niño, Mwinuka amesema wamevitaka vikundi vinavyonufaika na mikopo hiyo kusimamia vizuri shughuli zao na kuhakikisha mazao yanahifadhiwa katika maeneo salama yasiyokumbwa na mafuriko.

Amesema wafugaji pia wamepewa elimu kuhusu magonjwa hatari ya mifugo na umuhimu wa kutumia chanjo ili kuzuia milipuko ya magonjwa inayoweza kusababisha hasara katika shughuli zao.
Kwa upande wake, Happy Mwananjala, kutoka Kikundi cha Shujaa kilichopo Kata ya Utengule Usongwe, amesema kikundi hicho kimepata mkopo wa Sh10 milioni na kuahidi kuutumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
Amesema wanatarajia kutumia fursa hiyo kukuza shughuli zao za kiuchumi na kuboresha hali ya maisha ya wanachama.
Naye Lucynes Mbilinyi, mkazi wa Igoma ambaye ni mtu mwenye ulemavu, amesema amepata mkopo wa Sh4 milioni utakaomwezesha katika kilimo cha viazi mviringo.


More Stories
Bodi ya Wakurugenzi ETDCO yakagua miradi nyanda za Juu Kusini
Serikali yaweka mikakati kutekeleza ajenda ya sifuri Tatu
Tanzania,Uganda kuimarisha Biashara na Utalii Ziwa Victoria