Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Wizara ya Nishati pamoja na taasisi zake imetunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kufanikisha Mdahalo wa Nishati Safi ya Kupikia, uliofanyika Kizimkazi, Mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar, tarehe 11 Agosti 2026.
Tuzo hiyo imetolewa usiku wa tarehe 12 Agosti 2026 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan, na kupokelewa kwa niaba ya Wizara ya Nishati na taasisi zake na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba.
Mdahalo huo, uliokuwa na lengo la kujadili namna ya kuongeza kasi ya upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia iliyo endelevu, salama na nafuu kwa wananchi na taasisi, uliwakutanisha wadau mbalimbali kutoka Serikalini, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha, wanateknolojia, watafiti na asasi za kiraia.
Mdahalo huo uliandaliwa na Taasisi ya Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha na kuchagiza hatua za pamoja katika kuendeleza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Katika Mdahalo huo, Serikali iliendelea kusisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, taasisi za fedha na wadau wengine.
Tuzo hiyo ni ishara ya kutambua mchango na ushirikiano wa Wizara ya Nishati na taasisi zake katika kufanikisha Mdahalo huo, unaolenga kuchagiza mjadala na hatua madhubuti kuelekea kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.


More Stories
Gereza kwamngumi lamkabidhi aliyekuwa mfungwa vifaa vya ujenzi
FCC yaongeza mkakati kudhibiti bidhaa bandia
Prof.Kabudi ahimiza matumizi sahihi Alama za Taifa