Mwandishi: Ismail Mayumba
Unyanyasaji wa mtandaoni ni vitendo vya matumizi mabaya ya teknolojia vinavyolenga kumdhalilisha, kumtukana, kumfedhehesha au kumletea madhara ya kihisia mtu, taasisi au kikundi fulani kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali. Ni hali inayofanya matumizi ya mtandao kuwa chanzo cha huzuni, hofu na msongo wa mawazo badala ya kuwa sehemu ya kujifunza, kubadilishana mawazo na kujenga maendeleo.
Tatizo hili linaweza kumkumba mtu yeyote bila kujali nafasi yake katika jamii, cheo chake, hadhi yake au aina ya kazi anayofanya. Linaweza kumpata Rais, mwanasiasa, mwanamichezo, msanii, mfanyabiashara, polisi, mkulima au hata mwanafunzi. Kutokana na uwezo wa watu wengi kuficha utambulisho wao mtandaoni, baadhi yao hutumia fursa hiyo kufanya matusi, kejeli na kashfa wakijua kuwa si rahisi kutambulika au kuwajibishwa mara moja.
Watu maarufu na viongozi wa ngazi mbalimbali ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa unyanyasaji wa mtandaoni. Mara nyingi hukumbana na shutuma kali, matusi, kejeli na taarifa za uongo zinazolenga kuharibu taswira yao mbele ya jamii. Wakati mwingine watu hutengeneza habari za uzushi au picha za uongo ili kuendeleza ajenda zao bila kujali madhara ya kihisia au kijamii yanayoweza kumpata mhusika.
Wasanii pia hukumbwa sana na changamoto hii. Wapo wanaotukanwa, kudhalilishwa au hata kuibiwa utambulisho wao mtandaoni ambapo watu hutumia majina au picha zao kuchapisha maudhui yasiyofaa. Hali hii huwafanya baadhi yao kuishi katika sintofahamu na kushindwa kujua hatua sahihi za kuchukua, hasa pale ambapo idadi ya wanaowashambulia huwa kubwa sana.
Kwa upande wa wanamichezo, mara nyingi hushambuliwa na mashabiki wa timu pinzani. Wachezaji hutukanwa, kubezwa na kudhalilishwa kutokana na matokeo ya mechi au ushindani wa kimichezo. Ingawa wengi hudhani ni sehemu ya burudani au mzaha wa michezo, vitendo hivi vinaweza kuathiri afya ya akili na kuharibu morali ya mchezaji.
Viongozi wakuu wa nchi, hususan marais na viongozi wa kisiasa, hukutana na aina mbalimbali za unyanyasaji wa mtandaoni. Wapinzani wao wanaweza kutengeneza picha za kudhalilisha, kusambaza kejeli, au hata kuwahamasisha watu kutoa matusi na kashfa kwa kisingizio cha kutoridhishwa na sera au maamuzi yao. Ingawa kukosoa ni haki ya kidemokrasia, ukosoaji huo unapaswa kuwa wa staha na wenye kujenga, si wa matusi na udhalilishaji.
Wananchi wa kawaida pia hupitia mateso makubwa ya unyanyasaji wa mtandaoni, mara nyingi kutokana na kutokujua haki zao za kisheria na namna ya kujilinda. Wapo wanaorekodiwa au kupigwa picha bila ridhaa yao, kisha maudhui hayo kuchapishwa mtandaoni kwa lengo la kuwacheka au kuwavunjia heshima. Athari zake huwa kubwa; baadhi hupata msongo wa mawazo, huzuni kali, sonona, na wengine hufikia hatua za kufanya maamuzi mabaya kutokana na aibu na fedheha.
Unyanyasaji wa mtandaoni ni kitendo kiovu kisichokubalika katika jamii yoyote yenye ustaarabu. Hakuna anayepaswa kukubali kunyanyaswa kimya kimya. Teknolojia ya kisasa ina uwezo mkubwa wa kuwabaini watu wanaofanya vitendo hivyo hata kama wamejaribu kuficha utambulisho wao. Muhimu ni kwa mhanga kuwa jasiri, kuweka wazi ukweli pale inapobidi, kuhifadhi ushahidi wa unyanyasaji huo na kuruhusu sheria kuchukua mkondo wake.
Mara nyingi, haki inapopatikana, mhusika anayefanya unyanyasaji anaweza kuwajibishwa kisheria, kuomba radhi hadharani na hata kulipa fidia kwa madhara aliyosababisha. Hii husaidia kurejesha heshima ya mwathirika na kuwa fundisho kwa wengine wenye nia ya kufanya vitendo kama hivyo.
Kila mmoja wetu anapaswa kutumia mitandao kwa hekima, heshima na uwajibikaji. Mitandao ya kijamii inapaswa kuwa sehemu ya kujenga maarifa, kuelimishana na kujadili masuala yenye tija kwa maendeleo ya jamii. Kupinga unyanyasaji wa mtandaoni ni jukumu la kila mtumiaji wa teknolojia. Kwa kufanya hivyo, tutajenga mazingira salama ya kidijitali yenye kuheshimu utu wa kila mmoja na kuchochea maendeleo badala ya migogoro na maumivu.

More Stories
Ifahamu Shambulio la DoS na DDoS katika Usalama wa Mitandao
Uvunaji wa Data Mtandaoni
Jinsi Links Zinavyotumika Kwenye Wizi wa Mtandaoni