August 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kutoka Maabara hadi Sokoni: UDSM yabuni Saruji na Teknolojia rahisi za Ujenzi

Na Joyce Kasiki

CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinaendelea kugeuza tafiti na maarifa ya kisayansi kuwa bidhaa halisi zenye uwezo wa kutatua changamoto zinazokabili sekta ya ujenzi nchini.

Kupitia ubunifu wa watafiti wake, chuo hicho kimebuni bidhaa mbalimbali za kiteknolojia, zikiwemo NovaCem, DuraCem, DuraCem One A, Bentox na Flax, ambazo zina matumizi katika ujenzi wa majengo, barabara, viwanda na uzalishaji wa nishati safi.

Ubunifu huo unaleta matumaini mapya kwa Tanzania inayotafuta njia za kujenga miundombinu imara, yenye gharama nafuu na inayozingatia zaidi uhifadhi wa mazingira.

Akizungumza katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu, Mkurugenzi wa Idara ya Kemia wa UDSM, Dkt. Makungu Madirisha anasema ,bidhaa hizo ni matokeo ya tafiti zinazofanywa na wataalamu wa chuo hicho kwa lengo la kutafuta suluhisho la changamoto zinazolikabili Taifa.

NovaCem: Saruji mbadala yenye matumizi mengi
Miongoni mwa teknolojia zinazovutia ni NovaCem, saruji mbadala inayoweza kutumika katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali za ujenzi.

Kwa mujibu wa Dkt. Makungu, NovaCem inaweza kutumika kutengeneza bidhaa kama matofali na paving, hivyo kutoa fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa bidhaa za ujenzi kutumia teknolojia iliyobuniwa na watafiti wa ndani.

Kwa soko linalohitaji bidhaa nyingi za ujenzi kutokana na ongezeko la shughuli za ujenzi wa nyumba, majengo ya biashara na miundombinu, teknolojia kama NovaCem inaweza kuwa miongoni mwa bunifu zinazoweza kupewa nafasi zaidi katika sekta hiyo.

DuraCem: Teknolojia inayolenga kuongeza uimara wa barabara

Kwa upande mwingine, DuraCem imebuniwa kwa matumizi yanayohusiana moja kwa moja na ujenzi wa barabara.

Dkt. Makungu anasema DuraCem inaweza kutumika katika ujenzi wa tabaka la chini na tabaka la juu la barabara, jambo linaloifanya kuwa teknolojia yenye umuhimu katika jitihada za kuboresha ubora na uimara wa miundombinu ya barabara.

“DuraCem inatumika sana katika kujenga tabaka la juu na tabaka la chini la barabara. DuraCem One A ni kionjo kinachochanganywa na lami mbalimbali,” anasema.

Anaeleza kuwa matumizi ya teknolojia hiyo yanaweza kusaidia kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababisha barabara kuharibika mapema, ikiwemo mazingira yenye maji yaliyo karibu na uso wa ardhi.

DuraCem One A: Kionjo kinacholenga kuboresha matumizi ya lami

Katika mnyororo huo wa ubunifu, UDSM pia imebuni DuraCem One A, ambayo hutumika kama kionjo kinachochanganywa na lami katika mchakato wa ujenzi wa barabara.

Kwa wataalamu na wadau wa ujenzi wa barabara, teknolojia hiyo inaweza kuwa sehemu muhimu ya kutafuta suluhisho la changamoto zinazohusiana na uimara wa barabara, hasa katika maeneo yenye mazingira magumu.

Dkt. Makungu anasema miongoni mwa faida za teknolojia hizo ni uwezo wa bidhaa kutoshambuliwa kwa urahisi na chumvi pamoja na kuwa na uimara unaohitajika katika matumizi ya ujenzi.

Bentox: Suluhisho la kuziba nyufa
Ubunifu wa UDSM hauishii kwenye saruji na ujenzi wa barabara.

Chuo hicho pia kimebuni Bentox, bidhaa inayoweza kutumika katika kuziba nyufa na pia kuwa na matumizi katika baadhi ya shughuli za viwandani, ikiwemo utengenezaji wa vifungashio.

Teknolojia hiyo inaonyesha namna tafiti za chuo zinavyolenga kutengeneza bidhaa zenye matumizi zaidi ya eneo moja, hivyo kuongeza uwezekano wa kutumika katika sekta mbalimbali za uchumi.

Flax: Teknolojia inayolenga kuboresha ubora wa biogas

Katika eneo la nishati safi, UDSM imebuni pia Flax, teknolojia inayolenga kusaidia kuchuja biogas kwa kuondoa baadhi ya gesi zisizohitajika, zikiwemo carbon dioxide na hydrogen sulfide.

Kwa kufanya hivyo, teknolojia hiyo inalenga kuboresha ubora wa biogas na kuongeza thamani ya nishati inayozalishwa.

Ubunifu huu unaendana na mwelekeo wa dunia wa kutafuta nishati safi na teknolojia zinazoweza kupunguza athari za mazingira.
Kutoka maabara hadi soko: Changamoto bado ipo

Pamoja na ubunifu huo, UDSM inakabiliwa na changamoto ya kuzalisha bidhaa hizo kwa kiwango kikubwa ili kukidhi mahitaji ya soko.

Dkt.Makungu anasema kwa sasa baadhi ya teknolojia hizo bado zinazalishwa kwa kiwango kidogo kutokana na ukosefu wa vifaa vya kisasa vya uzalishaji.

Miongoni mwa vifaa vinavyohitajika ni mashine ya “flash cascade”, ambayo kwa mujibu wa Dk. Makongo inapatikana nchini China kwa gharama inayokadiriwa kufikia dola 200,000 za Marekani.

“Tunamini tukipata mashine kama hii itaweza kutusaidia kutoka tulipo na kwenda kwenye uzalishaji mkubwa na hivyo kuweza kukidhi mahitaji ya wateja wanaohitaji bidhaa hizi,” amesema.

Baadhi ya bidhaa hizo tayari zimeanza kutumika sokoni, hasa kwa watumiaji binafsi, huku baadhi ya taasisi za serikali zikionesha nia ya kuzitumia.
Wito kwa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS),Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini ( TARURA ) na wadau wengine.

Dkt. Makungu ametoa wito kwa wadau mbalimbali kushirikiana na watafiti ili teknolojia hizo zitoke katika uzalishaji mdogo na kufikia matumizi mapana zaidi nchini.

Miongoni mwa taasisi alizotaja ni TARURA, TANROADS, Wizara ya Nishati, Wakala wa Majengo Tanzania na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).

Ushirikiano wa aina hiyo, anasema, unaweza kusaidia kuunganisha utafiti wa vyuo vikuu na mahitaji halisi ya soko, huku ukifungua fursa kwa bidhaa zinazobuniwa nchini kutumika katika miradi mikubwa ya maendeleo.

Ubunifu unaolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Kwa mujibu wa Dkt. Makungu, teknolojia hizo haziangalii ujenzi pekee bali pia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Sekta ya ujenzi ni miongoni mwa sekta zinazohusishwa na uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa, hivyo watafiti wanaona umuhimu wa kutafuta teknolojia mbadala zinazoweza kupunguza athari hizo.

“Tanzania ikiwa sehemu ya jumuiya ya kimataifa, imesaini mikataba mbalimbali inayolenga kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hivyo tafiti na teknolojia zinazobuniwa nchini zinapaswa kuangalia namna ya kupunguza athari za uzalishaji wa hewa hizo,” anasema.

Anasema utafiti wa UDSM unaendelea kuangalia matumizi ya malighafi zinazopatikana nchini, sambamba na mnyororo mzima wa uchakataji.

“Utafiti huu unaenda sambamba na kutafuta masuluhisho ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Pia tunaangalia mnyororo mzima wa uchakataji, kwa sababu tunataka kutumia kwa wingi malighafi zinazopatikana hapa Tanzania,” anasema.

Fursa kubwa kwa wawekezaji na watumiaji wa bidhaa za ujenzi

Ubunifu huu unaweka mbele swali muhimu: Je, Tanzania iko tayari kugeuza utafiti wa vyuo vikuu kuwa bidhaa zinazotengenezwa kwa wingi na kutumiwa na soko la ndani?

Kwa UDSM, jibu linaonekana kuwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya watafiti, Serikali, taasisi za utekelezaji, wawekezaji na watumiaji wa mwisho.

Kwa wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa za ujenzi, teknolojia kama NovaCem, DuraCem na DuraCem One A zinaweza kuwa eneo la kuangalia kwa karibu kadiri uzalishaji wake unavyopanuka.

Na kwa Tanzania inayohitaji barabara imara, majengo bora, nishati safi na matumizi endelevu ya malighafi za ndani, bunifu hizi zinaonyesha kuwa suluhisho la baadhi ya changamoto za maendeleo linaweza kuwa tayari linapatikana ndani ya maabara za watafiti wa Kitanzania.

Changamoto kubwa sasa si kubuni pekee, bali ni kuvuka daraja kutoka maabara hadi kiwandani, kutoka kiwandani hadi sokoni, na kutoka sokoni hadi matumizi mapana ya kitaifa.