September 30, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kurudi Shuleni baada ya Ujauzito,Safari yenye Miiba

Na Penina Malundo,TimesMajira

THERESIA Juma mwenye umri wa miaka(21),hakuwahi kufikiria kuwa siku moja angeingia darasani akiwa mama wa mtoto.

Akiwa na miaka 18 na baada ya kumaliza kidato cha kwanza, Theresa alipata ujauzito uliokatiza safari yake ya elimu wakati akijiandaa kuingia kidato cha pili.

Kabla ya hapo, alikuwa amefaulu kwa Daraja la Kwanza Mtihani wake wa Darasa la Saba na alikuwa na matumaini ya kuendelea na masomo.

Lakini ujauzito ukabadilisha kila kitu na kufanya matumaini yake kuondoka na ndoto kufifia.

Anasimulia kuwa baada ya kupata ujauzito, alifukuzwa nyumbani na kuanza kupambana na maisha huku akijitafutia mahitaji yake mwenyewe.

“Nikikumbuka naumia sana….(Analia)… Niliacha shule nikiwa naingia kidato cha pili ambapo nilifaulu na kupata Daraja la Kwanza nilipopata ujauzito. Nilifukuzwa nyumbani na niliangaika sana,nimeamua kujitafutia maisha huku nikijisomesha mwenyewe nikiwa nalipa ada na kuendesha maisha yangu,”anasema.

Anasema anashindwa kuvaa nguo za shule kutokana na changamoto ya majirani kuona kama anachofanya hakipo sawa kwake.

”Nimekuwa nikienda shule nikivaa nguo za nyumbani kwa kuhofia kunyooshewa vidole na majirani zangu.

”Hivyo uwa naamua kuvaa nguo za kawaida na kwenda shule,na nikifika shuleni mtoto wangu uwa namuacha kwa Mwalimu muda wa mapumziko nakuwa naunga nae,”anasema

Leo Theresa yuko tena shuleni.
Tofauti ni kwamba sasa anaingia darasani akiwa na jukumu jingine la kulea mtoto wake.

Na hapo ndipo changamoto nyingine inaanza.Kwa Theresa, kurejea shuleni hakumaanishi tu kupata nafasi ya kukaa darasani. Ni safari ya kujaribu kusawazisha masomo, malezi na maisha yake binafsi huku akikabiliana na changamoto zinazowakabili wasichana wengine wanaorejea shuleni baada ya kukatisha masomo.

Hili ndilo tatizo ambalo limeanza kuibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa elimu na haki za mtoto wa kike ambapo wanajitokeza na kuhakikisha
wasichana wanaporejea shuleni, wanapata mazingira ya kuwasaidia kubaki shuleni hadi mwisho.

Mwaka 2013, nchi 55 ambazo zinaunda Umoja wa Afrika (AU) zilipitisha Ajenda 2063, mkakati wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa bara zima.

Katika mkakati huu, serikali za Afrika ziliweka dhamira ya kujenga “mtaji wa rasilimali watu” wa Afrika, ambao uliutambua kama “rasilimali yenye thamani zaidi,” kupitia uwekezaji endelevu katika elimu, ikiwa ni pamoja na “kuondokana na tofauti za jinsia katika ngazi zote za elimu.”

Miaka miwili baada ya kupitisha Ajenda 2063, serikali za Afrika ziliungana na nchi nyingine katika kupitisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs), ajenda ya maendeleo ambayo inalenga kuhakikisha kwamba “hakuna anaebaki nyuma,” ikiwa ni pamoja na ahadi ya kuhakikisha elimu jumuishi na bora kwa wote.

Serikali za Afrika vile vile zimepitisha malengo makubwa ya kumaliza ndoa za utotoni, kutambulisha elimu pana ya jinsia na afya ya uzazi, na kushughulikia kiwango kikubwa cha ujauzito wa utotoni barani kote ambao unaathiri vibaya elimu kwa mtoto wa kike.

Nchini Tanzania,Mwaka 2021, Waraka wa Elimu Na. 2 uliweka utaratibu unaoruhusu wanafunzi walioacha shule kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ujauzito, kurejea katika mfumo rasmi wa elimu.

Hatua hiyo ilitoa nafasi kwa wasichana waliokuwa wamekatisha masomo kuendelea na ndoto zao.

Lakini utekelezaji wake umeibua changamoto nyingine.

Kwa baadhi ya wasichana, kurudi shuleni kunamaanisha kuanza tena maisha ya elimu huku wakiwa wamebeba uzoefu wa ujauzito, kujifungua, malezi na wakati mwingine kukataliwa na familia au jamii.

Aidha, baadhi yao wanakutana na unyanyapaa kutoka kwa wanafunzi wenzao, jamii na wakati mwingine walimu.

Hali hiyo inaweza kuwafanya wajisikie tofauti na wengine na kupunguza ari ya kuendelea na masomo.

Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,Dkt. Gladness Kirei, anasema baadhi ya wanafunzi wanaoshindwa kuendelea na masomo wanakumbana na unyanyapaa unaowafanya wasijisikie vizuri.

Dkt. Kirei anatoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Kukabiliana na Changamoto ya Unyanyapaa kwa wanafunzi wanaorudi shuleni kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo ujauzito, iliyoanzishwa na Taasisi ya Msichana Initiative.

Kwa mujibu wa Dkt. Kirei,jamii inapaswa kuwa sehemu ya kuwasaidia wanafunzi hao badala ya kuwakatisha tamaa.

“Tunaipongeza Msichana Initiative kwa kuwapambania wasichana hadi kuona wale wanaokuwa na ujauzito wanarudi shuleni. Kupitia kampeni hii iliyozinduliwa leo, inaenda kuhamasisha jamii kuona kundi hili kama wanafunzi wengine na kuwaacha wasome ili kufikia ndoto zao,” anasema.

Unyanyapaa unavyoweza kuharibu safari ya pili

Msichana anaporejea shule baada ya kupata ujauzito, anahitaji zaidi ya sare, madaftari na nafasi ya kukaa darasani.

Anahitaji kukubalika,kuheshimiwa na zaidi ya yote, anahitaji mazingira ambayo hayatamkumbusha kila siku kuwa amewahi kukosea au kukumbana na changamoto fulani katika maisha yake.

Kwa baadhi yao, maneno ya kejeli kutoka kwa wanafunzi wenzao yanaweza kuwa mzigo mzito.

Kwa wengine, mtazamo wa jamii unaweza kuwafanya wajione hawastahili tena kuwa sehemu ya mazingira ya shule.

Dkt. Kirei anasema kuna umuhimu wa kuwasaidia wanafunzi hao kwa njia mbalimbali, ikiwemo mahitaji ya shule na kuwapa moyo ili waweze kufikia malengo yao.

Anasema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya elimu ili kuhakikisha wanafunzi, hususan watoto wa kike, wanapata elimu bora bila kunyanyapaliwa.

Aidha, anasema mwongozo unatoa nafasi kwa mwanafunzi anayekumbana na unyanyapaa kuweza kuhama shule endapo mazingira ya shule hiyo yanamfanya ashindwe kuendelea na masomo.

Msichana Initiative: Changamoto bado zipo

Mkurugenzi mpya wa Msichana Initiative, Consolata Chikoti, anasema taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kushughulikia changamoto zinazowakabili watoto wa kike.

Anasema utekelezaji wa Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 umekumbana na changamoto mbalimbali katika jamii.

Moja ya changamoto hizo ni unyanyapaa kwa wanafunzi wanaorejea shuleni baada ya kukatisha masomo.

“Utekelezaji wa Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 unaoruhusu kurejea shuleni kwa wanafunzi walioacha shule kutokana na sababu zozote zile, ikiwamo mimba, kurudi katika mfumo rasmi wa elimu, umekuwa na changamoto mbalimbali wanazopata katika jamii,” anasema.

Kwa mujibu wa Chikoti, taasisi hiyo imekuwa ikiona vikwazo vinavyomkabili mtoto wa kike na imekuwa ikijitahidi kuvitatua kupitia miradi mbalimbali.

Kupitia mradi wa Rudi Shule, taasisi hiyo imewafikia zaidi ya wasichana 500 na mwaka huu inalenga kuwafikia wanafunzi 250.

Lakini uzoefu wa utekelezaji wa mradi huo umeonyesha kuwa changamoto haipo tu kwenye kurejesha wasichana shuleni.

“Tumegundua katika utekelezaji wa mradi huo kwamba wasichana wanakumbana na changamoto ya unyanyapaa pale wanaporudi shuleni kutoka kwa wanafunzi wenzao, jamii na wakati mwingine kwa walimu,”anasema.

Sauti za wasichana zipewe nafasi

Mwaka 2026, Ajenda ya Msichana inaingia katika toleo lake la tisa ikiwa na kaulimbiu “Kuinua Sauti za Wasichana kwa Maendeleo Endelevu.”

Jukwaa lililoanzishwa mwaka 2017 mjini Dodoma na kwa kipindi cha miaka tisa limehusisha zaidi ya wasichana na wanawake vijana 15,000 kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Mwaka huu,zaidi ya wasichana 5,000 wanatarajiwa kushirikishwa kupitia matukio mbalimbali katika shule na jamii zao,huku takribani wasichana 200 wakitarajiwa kushiriki katika kilele cha jukwaa jijini Dar es Salaam.

Lengo ni kuhakikisha wasichana hawabaki kuwa watazamaji wa mijadala inayowahusu bali wanapaswa kuzungumza,kusikilizwa huku mawazo watakayoyatoa yanapaswa kufika kwa wazazi, walimu, taasisi na watoa maamuzi.

Kwa sababu msichana aliyepitia ujauzito na kurejea shuleni ndiye anayejua kwa karibu zaidi changamoto anazokutana nazo.

Changamoto bado ipo

Hadithi ya Theresa inaonyesha kuwa nafasi ya pili inaweza kubadili maisha ya msichana.

Lakini nafasi hiyo inahitaji kuambatana na msaada.

Kumrudisha msichana shuleni bila kushughulikia unyanyapaa, changamoto za malezi, mahitaji ya shule na mazingira yanayomzunguka kunaweza kufanya safari yake kuwa ngumu zaidi.