August 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Tanga kujiandaa kupokea Gesi Asilia kwa matumizi

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

MKOA wa Tanga umetakiwa kujiandaa kwa ujio wa gesi asilia kwa matumizi mbalimbali, ikiwemo kupikia na shughuli za uzalishaji wa joto, huku Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) likiendelea na mipango ya kuifikisha nishati hiyo mkoani humo.

Hayo yamesemwa leo Agosti 19,2026 na Hassan Temba kutoka TPDC wakati wa Wiki ya Kitaifa ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu  yanayofanyika mkoani Tanga.

Temba amesema gesi asilia haipaswi kuonekana kama chanzo cha uzalishaji wa umeme pekee, bali ina matumizi mbalimbali yanayoweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuongeza fursa za uwekezaji nchini.

Amesema mpango wa kuifikisha gesi asilia mkoani Tanga unaendelea, hivyo wananchi wanapaswa kujiandaa kutumia fursa zitakazotokana na upatikanaji wa nishati hiyo.

“Gesi asilia haitumiki kwa ajili ya umeme pekee,pia hutumika kwa ajili ya kupikia na shughuli zinazohitaji joto,hivyo Tanga inapaswa kujiandaa kwa fursa hii,” amesema Temba.

Kwa mujibu wa Temba, gesi asilia pia inaweza kutumika kama malighafi katika uzalishaji wa mbolea, hatua ambayo inaweza kufungua fursa zaidi za uwekezaji katika sekta ya viwanda.

Amesema TPDC inaendelea na mipango ya kuendeleza matumizi hayo na inaamini kuwa katika siku zijazo kutakuwa na viwanda vya uzalishaji wa mbolea vitakavyotumia gesi asilia kama sehemu ya malighafi.

Aidha, amesema sekta ya gesi asilia ina fursa kubwa kwa wawekezaji binafsi, ikiwemo uanzishwaji wa vituo vya kujaza gesi asilia kwa magari pamoja na kushiriki katika mnyororo mzima wa usambazaji wa nishati hiyo.

Temba amesema kampuni mbalimbali tayari zinashiriki katika shughuli za usambazaji wa gesi asilia, akitolea mfano kampuni ya Puma, huku akizialika kampuni nyingine kuingia katika sekta hiyo ili kuongeza upatikanaji wa gesi kwa watumiaji mbalimbali.

Amesema ushiriki wa sekta binafsi katika usambazaji na matumizi ya gesi asilia unaweza kuwa fursa muhimu ya biashara na uwekezaji, sambamba na kuongeza matumizi ya nishati safi nchini.

Akizungumzia ushiriki wa TPDC katika Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Temba amesema shirika hilo limetumia maonesho hayo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu teknolojia zinazotumika katika utafutaji, uendelezaji na usambazaji wa mafuta na gesi asilia nchini.

Amesema wananchi wanaotembelea banda la TPDC wanapata fursa ya kujifunza kuhusu gesi asilia, namna mafuta yanavyopatikana, maeneo yanayofanyiwa utafutaji pamoja na hatua ambayo Tanzania imefikia katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia.

Temba amewahimiza wananchi na wawekezaji kutembelea banda la TPDC katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi kuhusu matumizi na fursa zinazopatikana katika sekta ya mafuta na gesi asilia.