August 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Nungu: Ujuzi wa vitendo msingi wa kuwaandaa vijana

Na Joyce Kasiki, Tanga

MKURUGENZI Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Dkt.Amos Nungu amesema Watoto na vijana wanapaswa kupewa elimu inayowawezesha kujifunza kwa vitendo ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha na kutumia maarifa yao kutengeneza suluhisho za matatizo yanayoikabili jamii.

Dkt.Nungu amesema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika banda la COSTECH wakati wa maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga.
Amesema elimu ya vitendo ina nafasi muhimu katika kumwandaa mwanafunzi kuwa na uwezo wa kutumia maarifa anayojifunza darasani katika mazingira halisi.

Kwa mujibu wa Dkt. Nungu, kuwajengea watoto msingi wa ujuzi na ubunifu tangu hatua za awali za elimu kutawasaidia kuwa wabunifu na wenye uwezo wa kutafuta majibu ya changamoto zinazowazunguka.

Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na taasisi mbalimbali za kuwawezesha kukuza vipaji, ujuzi na bunifu zao badala ya kusubiri fursa ziwafuate.

“Tunapokuwa na vijana wenye bunifu, tunapaswa kuwapa nafasi na kuwaunga mkono ili waweze kufikia malengo yao,” amesema Dk. Nungu.

Ameeleza kuwa COSTECH inaendelea kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupata ushauri, maelekezo na fursa za kuendeleza bunifu zao hadi kufikia hatua ya kutumika katika jamii.

Dkt. Nungu amesema mashauriano kati ya wabunifu na taasisi zinazohusika ni muhimu kwa sababu yanawawezesha vijana kupata mwongozo unaofaa kuhusu namna ya kuboresha na kuendeleza bunifu zao.

Amesema matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kutatua changamoto za wananchi, kuongeza fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Aidha, amewataka vijana kuwa tayari kujifunza na kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza ujuzi na uwezo wa kubadilisha mawazo yao kuwa bunifu zinazoweza kuleta manufaa kwa jamii.

Amesisitiza kuwa juhudi za kuwaandaa vijana zinapaswa kuanzia katika ngazi za chini za elimu kwa kuwapatia fursa za kusoma, kusikia na kujifunza kwa vitendo.

Kwa mujibu wa Dkt. Nungu, mazingira bora ya elimu, ujuzi na ubunifu yatawezesha kujenga kizazi chenye uwezo wa kutumia maarifa na teknolojia kutengeneza suluhisho za changamoto za sasa na zijazo.