September 27, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Equity Bank yaongeza nguvu sekta ya Madini Tanzania

Na Joyce Kasiki, Geita

WADAU wa sekta ya madini nchini wanaweza kupata fursa mbalimbali za kifedha kupitia Equity Bank Tanzania, ikiwemo mikopo, mitaji ya biashara, pamoja na uwezeshaji wa upatikanaji wa mitambo na vifaa vinavyohitajika katika shughuli za uchimbaji na biashara za madini.

Kauli hiyo imetolewa leo, Septemba 27, 2026, na Mkuu wa Idara ya Biashara—Wateja Wadogo, wa Kati na Binafsi wa Equity Bank Tanzania, Theresia Aloyce Mayanie, wakati wa Maonesho ya Tisa ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, mkoani Geita.

Mayanie amesema benki hiyo inalenga kuwafikia wadau katika maeneo mbalimbali ya mnyororo wa thamani wa madini, wakiwemo wachimbaji wadogo, wafanyakazi wa migodini na biashara zinazohusiana na madini hadi kwa watumiaji wa mwisho.

Amesema kupitia huduma hizo, wadau wanaweza kupata mitaji ya kuendesha shughuli zao, kununua vifaa na mitambo ya kazi, pamoja na kuongeza thamani ya bidhaa zinazotokana na shughuli za madini.

“Tumelenga kuwafikia wadau wote waliopo katika mnyororo wa thamani wa madini ili waweze kupata huduma zinazowawezesha kukuza shughuli zao,” amesema.

Kwa upande mwingine, benki hiyo imesema wafanyakazi wanaohusika katika sekta ya madini pia wanaweza kutumia huduma za mikopo kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao mbalimbali ya kifedha.

Mbali na mikopo, Mayanie amesema Equity Bank Tanzania imekuwa ikitoa elimu ya fedha kwa wadau wa sekta hiyo, ikiwemo usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu za kifedha na namna ya kupanga uwekezaji kwa ajili ya mahitaji ya baadaye.

Amesema elimu hiyo inalenga kuwasaidia wadau kuwa na misingi mizuri ya kifedha na kujenga biashara zinazoweza kuendelea kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine, Mayanie amewaalika Naibu Waziri pamoja na wananchi na wateja wanaotembelea maonesho hayo kufika katika banda la Equity Bank Tanzania kwa ajili ya kupata maelezo kuhusu huduma na suluhisho za kifedha zinazolenga sekta ya madini.