Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online,Arusha
KAMATI ya Wataalamu wa Serikali ya Maandalizi ya Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), imekagua miundombinu mbalimbali katika Jiji la Arusha ikiwa ni sehemu ya kuimarisha maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa michuano hiyo.

Ukaguzi huo umelenga kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, kubaini changamoto na kutoa msukumo kwa wadau, wakandarasi na kampuni zinazotekeleza miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Katika ziara hiyo, kamati imetembelea na kukagua viwanja vya mazoezi vya Mgambo, Engutoto na Kisongo, pamoja na Uwanja Mpya wa Arusha unaojumuisha viwanja viwili vya ziada vya mazoezi (Annex 1 na Annex 2).

Aidha, kamati imekagua mradi wa ujenzi na maboresho ya sehemu ya kupumzika wageni ya Themi (Themi Living Garden), ujenzi wa barabara zinazounganisha maeneo mbalimbali na Uwanja Mpya wa Arusha, ikiwemo Barabara ya Mbauda–Losinyai na Mateves–Bondeni, kwa lengo la kufuatilia maendeleo ya ujenzi na maandalizi ya miundombinu ya usafiri kuelekea uwanjani.
Kamati hiyo inajumuisha wataalamu kutoka wizara na taasisi mbalimbali za Serikali, ambao wana jukumu la kuratibu, kufuatilia na kushauri kuhusu utekelezaji wa maandalizi ya miundombinu na huduma muhimu zitakazohitajika wakati wa michuano ya AFCON 2027.




More Stories
Equity Bank yaongeza nguvu sekta ya Madini Tanzania
Watoto waathirika wa moyo, jamii yatakiwa kutambua dalili
Magu yashauriwa kuainisha shule zenye elimu jumuishi