Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
WAKAZI na wafanyabiashara wa Kahama mkoani Shinyanga wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha kwa urahisi zaidi, kufuatia Yas Tanzania kufungua duka jipya mjini humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa duka hilo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mataluma Kaniki ali
amesema kuendelea kuongezeka kwa uwekezaji wa sekta binafsi ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira katika Manispaa hiyo.
“Kahama ni miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi kiuchumi kutokana na shughuli za madini, kilimo na biashara. Tunapopata uwekezaji kama huu, tunaona matokeo yake si katika huduma pekee, bali pia katika ajira, biashara zinazozunguka uwekezaji huo na mchango wake katika uchumi wa Manispaa yetu. Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri yatakayovutia uwekezaji zaidi Kahama,” amesema Kaniki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas Tanzania, Mwangaza Matotola amesema duka hilo limefunguliwa ili kuwapa wateja wa Kahama sehemu ya kupata huduma na msaada wanaouhitaji kwa urahisi zaidi.
“Tunataka mteja wa Kahama apate huduma anayoihitaji kwa urahisi na kwa wakati.
Duka hili linatupa nafasi ya kuwa karibu zaidi na wateja wetu, kusikiliza mahitaji yao, kutatua changamoto zao na kuwapatia huduma za Yas na Mixx katika sehemu moja,” amesema Matotola.
Amesema, duka hilo ni sehemu ya mtandao wa zaidi ya maduka 556 ya Yas nchini, yanayowezesha wateja kupata huduma mbalimbali ikiwemo za laini, intaneti, vifaa vya mawasiliano na huduma za kifedha.
Matotola amesema, upanuzi wa maduka unaenda sambamba na uwekezaji wa zaidi ya Sh trilioni moja ambao Yas imefanya katika kupanua na kuboresha miundombinu na huduma zake nchini.
Kwa mujibu wake, Yas kwa sasa ina zaidi ya minara 4,900, inayowezesha huduma za teknolojia za 4G na 5G katika maeneo mbalimbali, huku ikihudumia zaidi ya wateja milioni 33.2 Tanzania Bara na visiwani.
Amesema, uwekezaji katika mtandao na vituo vya huduma kwa wateja unalenga kuhakikisha ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali.

More Stories
Azania yatoa mikopo ya Sh5 bilioni kwa wachimbaji
Kamati ya serikali yakagua miundombinu kuelekea AFCON 2027
Equity Bank yaongeza nguvu sekta ya Madini Tanzania