Na Joyce Kasiki, Dodoma
OFISI ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na wilaya imetoa kifuta jasho cha Sh500,000 kwa kila mmoja wa wafanyabiashara 44 walioathirika na moto ulioteketeza vizimba na mali zao katika Soko la Machinga jijini Dodoma usiku wa kuamkia Septemba 21, 2026.
Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, kutembelea soko hilo jana kwa ajili ya kuwafariji wafanyabiashara walioathirika, ambapo pia ameagiza ukarabati na urejeshaji wa miundombinu katika eneo lililoathiriwa kukamilishwa ndani ya siku 10 ili kuwawezesha kurejea katika shughuli zao kwa haraka.
Amesema Serikali imeunda timu ya haraka ya kufanya tathmini ya uharibifu uliotokea katika soko hilo na kubaini mahitaji ya kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.
Kwa mujibu wa Senyamule, uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha moto huo ni hitilafu katika mfumo wa umeme iliyotokana na uunganishaji wa umeme usiozingatia viwango, hali iliyosababisha nyaya kugusana katika vizimba vilivyojengwa kwa PVC na mbao nyepesi katika eneo la Block C.
Amesema baadhi ya watu walikuwa wakitumia nyaya za umeme wa sola kuunganisha umeme wa TANESCO, jambo ambalo liliongeza hatari ya kutokea kwa hitilafu katika mfumo wa umeme.
Moto huo ulisababisha vizimba 20 kuungua pamoja na mali zilizokuwamo, huku wafanyabiashara 44 wakitajwa kuathirika.
Senyamule amesema timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na viongozi wa soko itaundwa kwa ajili ya kupitia na kuboresha miundombinu ya soko, ikiwemo mifumo ya umeme, usalama dhidi ya moto, ujenzi na mpangilio wa vizimba.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha tatizo la uunganishaji wa nyaya na matumizi ya vifaa visivyo na viwango halijirudii, pamoja na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa majanga kama hayo siku zijazo.
Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara kutounganisha nyaya za umeme kiholela na kuhakikisha maboresho ya vizimba yanafanyika kwa kufuata utaratibu uliowekwa na Jiji la Dodoma pamoja na viwango vya kitaalamu.
Katika mikakati ya muda mrefu, Senyamule amesema Jiji la Dodoma linatarajia kuanza haraka ujenzi wa eneo jingine la Soko la Machinga ili kupunguza msongamano wa wafanyabiashara katika soko hilo.
Amesema Jiji tayari limetenga shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa ujenzi huo.
Senyamule pia amezitaka benki pamoja na Jiji la Dodoma kuendelea kuwaunga mkono wafanyabiashara walioathirika kwa kuwawezesha kupata mitaji ili waweze kurejea na kuendelea na shughuli zao za biashara.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa Block C, Balozi wa eneo hilo, Abogast Assenga, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kuwafikia na kuwapa pole pamoja na hatua zilizochukuliwa kuwasaidia wafanyabiashara walioathirika na moto huo.

More Stories
OMTZD yakamilisha mipango ya kukabiliana na mafuriko Dar es salaam
Filamu ya The Rhinos of Ngorongoro yazinduliwa
Wananchi Matongo Mara kupata fidia