May 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Macho, masikio kwa Rais Samia Mei Mosi

*Wafanyakazi wasubiri kwa shauku nyongeza ya mishahara, malipo ya malimbikizo, kikokotoo kuibuka, TUCTA nayo matumaini ‘kibao’

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline

WAKATI RAIS Samia Suluhu Hassan, akitajiwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kitaifa katika Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, wafanyakazi nchini yanasubiri kwa shauku hotuba ya kiongozi huyo ili kujua mwelekeo wa maslahi yao.

Miongoni mwa mambo ambayo wafanyakazi wanatarajia Rais Samia kuyazungumza ni maboresho zaidi ya maslahi ya wafanyakazi, ikiwamo mishahara na uondoaji wa vikwazo vya ustawi wao.

Maadhimisho hayo yanafanyika Jumatano, Mei 1, 2024. Eneo lingine ambalo wafanyakazi wanasubiri kwa hamu kujua ni kuhusu kikokotoo cha mafao kwa wastaafu ambacho kimekuwa kikilalamikiwa mara kwa mara na wafanyakazi pamoja na wanasiasa.

Hivi karibuni Serikali imesema kuwa utumishi wa umma ni nguzo muhimu katika uendeshaji na uendelezaji wa nchi na wameendelea kutoa mchango ulioiwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi wa kipato cha kati cha kiwango cha chini.

Serikali imekuwa na matarajio makubwa na mchango wa watumishi wa umma katika maendeleo na ndio unaotarajiwa kuiwezesha nchi kufikia uchumi wa kati wa kiwango cha juu.

Maendeleo hayo yanatarajiwa kuongezeka kwa kuimarisha uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu kama inavyobaishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano Awamu ya Tatu.

Kwa upande wake Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeeleza matarajio yake ya kuwepo kwa ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi nchini kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Matarajio hayo yamekuja, baada ya Rais Samia kukubali kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitaifa, yanayotarajia kufanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Mei 1, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari hivi karibuni Rais wa TUCTA ucta, Tumaini Nyamhokya, alisema kutokana na vikao mbalimbali walivyofanya na Serikali, wamepitisha kaulimbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu kuwa ‘Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha.

Nyamhokya alisema maandalizi yote kuelekea sherehe hizo yamekamilika na maboresho makubwa yanaendelea katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

“Serikali ndio mwajiri namba moja, ndio maana tuna matarajio makubwa kwa Rais kutoa neno jingine la kuleta ahueni ya maisha kwa wafanyakazi katika maadhimisho ya mwaka huu,” alisema Nyamokya.
Alisema wanayo matarajio makubwa ya kupandishiwa kiwango cha mishahara kwa ajili ya kuboresha maisha ya wafanyakazi nchini kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha na kipato kisichokidhi mahitaji ya kila siku ya mfanyakazi.

“Lakini pia sisi kama watetezi wa masilahi ya wafanyakazi ni jukumu letu kuikumbusha Serikali na waajiri wetu juu ya mambo haya, kuwa mishahara ikiwa bora itawezesha mafao kuwa bora tukiwa kazini na wakati wa kustaafu,” alisema.

Aliwataka wafanyakazi wote walioko Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kuhudhuria sherehe hizo kwa wingi ili kuonyesha umoja wao.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti (RAAWU), Jane Mihanji amesema maadhimisho hayo mbali na kutetea masilahi ya wafanyakazi, pia wanalenga kuwahimiza wanachama wao kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi ili kuleta tija iliyokusudiwa.

“Tunapodai masilahi mazuri, lazima tuonyeshe kwa nini tunadai na njia ni moja tu, kutekeleza wajibu wetu kwa kuchapa kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa, ndio maana lazima tukutane kwa pamoja tukumbushane hayo,” alisema.

Alisema chimbuko la maadhimisho hayo ni kukumbuka madhila ya wafanyakazi waliyoyapata miaka ya zamani wakati wa mapinduzi ya viwanda wakitegemea haki zao, ambapo baadhi yao waliuawa na wengine wakateseka.