May 15, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC.Lulandala:Miaka 60 ya Muungano na mafanikio lukuki

Na Mary Margwe, Simanjiro

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara Fakii Raphael Lulandala amesema
Tanganyika na Zanzibar imesheherekea miaka 60 ya Muungano nchi ikiwa na mafanikio mbalimbali ikiwemo ya miundombinu ya barabara.

Ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan serikali imefanya shughuli nyingi za kuiletea nchi mafanikio ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali ikiwemo Simanjiro.

Akizungumza Aprili 26,2024 kwenye Kilele cha maadhimisho ya siku ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofayika kimkoa wilayani Simanjiro, Mkuu huyo wa Wilaya amesema katika kipindi hicho kwa upande wa sekta ya elimu kuna madarasa mengi na yenye ubora,sekta ya afya karibia kila Tarafa ina kituo cha afya,hospitali za Wilaya na hospitali za Mkoa.

Sanjari na hayo Lulandala amesema pamoja na kwamba bado kuna uhitaji wa maji lakini Mamlaka za maji zinafika mahali husika kupeleka maji ” Tunasheherekea miaka 60 ya Muungano tukiwa tumeshuhudia mafanikio makubwa”.

“WanaManyara tunaunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali katika kuiendeleza, kudumisha na kuimarisha Muungano wetu, pia tunaendelea kuwa wasimamizi wazuri wa shughuli zote za miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha ulinzi,usalama na amani vinaendelea kuwepo miongoni mwa wananchi wetu,”ameeleza Lulandala.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Manyara Maryam Muhaji ameitaka jamii kuhakikisha wanaimarisha Muungano pamoja na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia unayoendelea mkoani humo.

Kufuatia uwepo kwa vitendo hivyo ndani ya Mkoa huo amewaomba viongozi wa dini kanisani na misikitini suala la ukatili wa kijinsia iwe ndio agenda ya kukemea.

Naye Katibu wa Siasa , Itikadi na Mafunzo Mkoa wa Manyara John Nzwalile amesema zipo faida nyingi za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hivyo kuwaomba Watanzania kutoruhusu watu kuubeza.

Nzwalile amesema Muungano ndio maisha.na mafanikio yote yanayoonekana yamefanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania ( UWT ) Wilaya ya Simanjiro Anna Shinini amesema Muungano huo umeendelea kuwaunganisha wakina mama kwa umoja wao na kuwapa nguvu, ujasiri mkubwa wa kufanya kazi hususani kupitia nafasi ya Rais Samia kama mwanamke shupavu, mahili katika kuliongoza Taifa kama Rais.

“Mimi kama Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Simanjiro namuunga mkono mama yetu mchapakazi Samia ambaye ni mwanamke aliyetujengea ujasiri mkubwa na sisi tunamuumga mkono kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuendelea kumtia moyo katika Utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku,”amesema.

Sanjari na hayo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kurudisha mikopo ya asilimia 10 iliyokua ikitolewa na Halmashauri nchini kupitia mapato yake ya ndani kwani ilikuwa msaada kwa walengwa kuwaondoa katika wimbi la umaskini na kuwainua kiuchumi.

Pia amewataka wanaochukua mikopo kuweza kuhakikisha inawanufaisha kisawa sawa ikiwa ni sambamba na kurudisha fedha hizo Kwa wakati ili kuwasaidia na wengine.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) ) Wilaya ya Simanjiro Timothy Ngoyai Mollel amesema Muungano umeendelea kuimarisha umoja na ushirikiano baina ya Tanganyika na Zanzibar.

” Kupitia Muungano pia tumeendelea kujifunza kazi kubwa zinazotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi mingi na mikubwa hapa nchini, lakini pia hata katika Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro nayo imeendelea kupata miradi mingi na mikubwa,”.