May 17, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Somalia kushirikiana na MSD ununuzi wa dawa

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraDar

RAIS wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud amesema nchi yake imeamua kushirikiana kwa karibu na Bohari ya Dawa (MSD) kwa kununua bidhaa za afya na kubadilishana uzoefu wa namna mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya unavyofanya kazi.

Rais Mahamud ameyasema hayo alipoitembelea MSD, na kuongeza kuwa kutokana na uzoefu wa MSD, wana uhakika kuwa ubora wa bidhaa za afya utakuwa wa uhakika.

Naye Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kwa kuwa Somalia ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Tanzania kupitia MSD itaweza kununua bidhaa za afya kwa pamoja ili kupata bidhaa hizo kwa bei nafuu.

Ameongeza kuwa, Marais wa nchi hizo mbili, yaani Tanzania na Somalia wamewapa maelekezo Mawaziri wa Afya ili nchi zao kukaa pamoja na kuangalia namna ya kushirikiana katika masuala ya upatikanaji wa bidhaa za afya kwa urahisi, kuzingatia ubora na kwa bei nafuu.

Rais huyo wa Somalia na ujumbe wake walizungumza na viongozi wa Wizara ya Afya, Menejimenti ya MSD na kutembelea ghala la kuhifadhia dawa la makao makuu MSD.