Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Sengerema
MKURUGENZI wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA), Walter Miya, amesema changamoto kubwa walioibaini katika jamii ni ukosefu wa elimu kuhusu matumizi ya unga uliorutubishwa pamoja na uwepo wa mashine chache za urutubishaji vyakula,hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini mbali na miji.
Miya ameeleza Mei 19,2026 wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kubaini na kuwapa rufaa watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi, Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii(CHWs) 25 kutoka Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza.

Ambapo kupitia mafunzo hayo baadhi ya wahudumu hao kutoka maeneo ya pembezoni mwa mjini wilayani humo,wahawahamu uwepo wa alama au unga uliorutubishwa na kuongezewa madini ya folic acid,jambo linaloonesha umuhimu wa kuongeza juhudi za utoaji elimu kwa jamii.
Miya amesema ipo haja ya wadau wa lishe na urutubishaji kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wahudumu wote wa afya ngazi ya jamii kwa kuwa ndio wanaowafikia wananchi katika kaya nyingi zinazotumia unga wa mahindi unaosagwa kienyeji ili kuweza kupunguza au kumaliza changamoto ya kuzaliwa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Ameipongeza Serikali kwa kuweka sheria ya urutubishaji wa vyakula na mfumo wa vifungashio, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuboresha afya ya jamii huku akiwasisitiza kuwa ni muhimu kuongeza mashine za kurutubisha unga hususani vijiji,akitokea mfano wananchi wengi wa Sengerema husaga mahindi yao wenyewe badala ya kununua unga uliokwisha fungashwa madukani.Â
Kwa mujibu wa taarifa alizopata, Wilaya ya Sengerema ina mashine mbili tu za urutubishaji, hali inayosababisha wananchi wengi kushindwa kupata unga wenye virutubishi muhimu vya kusaidia kuzuia changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa watoto.

Kwa upande wake, Ofisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Neema Sappy,amesema Serikali inaendelea na mpango wa kufunga mashine za urutubishaji wa unga kwa kuongeza madini ya folic acid, ambayo ni muhimu katika kusaidia kuzuia changamoto hizo kwa watoto.
Sappy amesema kwa sasa Wilaya ya Sengerema ina mashine mbili zinazofanya kazi ya kurutubisha na kufungasha unga, huku wananchi wengi wakiendelea kusaga mahindi yao wenyewe badala ya kununua unga uliokwisha fungashwa.Halmashauri inaendelea kuhamasisha matumizi ya unga uliorutubishwa pamoja na matumizi ya vidonge vya folic acid vinavyotolewa katika vituo vya afya.
Ameongeza kuwa wanawake wanashauriwa kutumia vidonge vya folic acid miezi mitatu kabla na baada ya kupata ujauzito pamoja na kuwahi kliniki ndani ya wiki 12 za ujauzito ili kusaidia kuwakinga watoto dhidi ya kuzaliwa na changamoto ya kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Naye CHW kutoka Kata ya Buzilasoga wilayani Sengerema, Magdalena Lushosha,amesema ataenda kutoa elimu ya lishe kwa jamii kwa kutembelea kaya, mikutano ya hadhara.
“Vyakula jamii inayo nadhani changamoto ni mashine zinazotumika kuongeza virutubisho kwenye unga ndio hazipo.Hivyo Serikali ifanye jitihada za kuhakikisha mashine hizo zinakuwepo katika maeneo mengi hasa ya vijijini,”amesema Lushosha.
“Serikali ituletee mashine ili mwananchi akienda kusaga haongezewe na virutubisho hivyo ili tuondokane na changamoto ya mtoto kuzaliwa na mgongo wazi,”amesema Hilali Rusule CHW kutoka Kata ya Nyampulukano wilayani Sengerema.



More Stories
Wateja wa Exim kupata huduma za kibenki kupitia Whatsap
Serikali yaendelea kuboresha Sekta ya Elimu nchini
Yas yaongeza minara miwili ya 5G Arusha