May 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yaongeza minara miwili ya 5G Arusha

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

WAKAZI wa jiji la Arusha wanatarajiwa kunufaika na huduma bora zaidi za mawasiliano na intaneti yenye kasi kufuatia nyongeza ya minara miwili ya 5G kutoka Kampuni ya mawasiliano ya Yas jijini humo.

Uwekezaji huo umeongeza idadi ya minara ya 5G ya Yas kufikia 15 jijini humo huku ikiwa na jumla ya minara (20) ya 4G.

Uzinduzi huo ni muendelezo wa kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya kisasa zinazolenga kurahisisha shughuli za wananchi na kuchochea maendeleo ya kidigitali katika sekta mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Yas Kanda ya Kaskazini, Robert Sanyagi amesema kampuni hiyo imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya mawasiliano.

Lengo likiwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma zenye kasi, uhakika na viwango vinavyokidhi mahitaji ya dunia ya sasa inayotegemea teknolojia.

“Tunafahamu kuwa huduma bora za mawasiliano zina mchango mkubwa katika kukuza biashara, elimu, afya na huduma za kifedha.

“Kupitia minara hii mipya, wakazi wa Arusha watanufaika na matumizi bora zaidi ya intaneti yatakayorahisisha shughuli zao za kila siku,” amesema Sanyagi.

Amesema, teknolojia ya 5G itaongeza ufanisi kwa wafanyabiashara wanaotegemea miamala ya kidigitali, vijana wanaojifunza mtandaoni pamoja na wananchi wanaotumia huduma mbalimbali kupitia intaneti.

Kwa upande wake, mkazi wa Arusha, George Shirima amesema uwekezaji huo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya jiji hilo kutokana na ongezeko la matumizi ya huduma kidigitali katika shughuli za kila siku.

“Kwa sasa karibu kila kitu kinategemea intaneti, hivyo huduma bora ya mtandao itasaidia sana biashara kukua na vijana kupata fursa zaidi kupitia teknolojia.

” Huu ni uwekezaji wenye manufaa makubwa kwa wananchi wa Arusha,” amesema, Shirima.

Yas inaendelea kujivunia kuwa miongoni mwa kampuni zinazoongoza kwa uwekezaji wa teknolojia nchini ikiwa na zaidi ya minara 4,800 Tanzania nzima.

Kampuni hiyo imesema itaendelea kupanua huduma zake za 4G na 5G ili kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata mawasiliano ya uhakika na yenye viwango vya kimataifa.