Na Mwandishi Wetu,Timesmajira
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya, ameutaka uongozi na wataalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa wakati unaofaa ili kuendana na misimu ya kilimo na kuongeza uzalishaji.
Millya ametoa maagizo hayo alipotembelea banda la TFRA lililopo katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma.
Amesema TFRA inapaswa kutekeleza kwa ufanisi maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa kilimo nchini.

“Katika eneo ambalo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka nguvu nimeona bajeti ya kilimo imekuwa ikiongezeka sana. Hivyo nawaomba mtekeleze maono hayo kwani Serikali haiwezi kufanya bila nyinyi, hivyo naomba muwasaidie wakulima,” amesema Millya.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti wa TFRA, Happiness Mbelle, amesema mamlaka hiyo inalenga kufikia mwaka 2030 ikiwa imepunguza kwa kiwango kikubwa utegemezi wa mbolea zinazoagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema lengo hilo litafikiwa kupitia kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji na kuhamasisha uanzishwaji wa viwanda vya kuzalisha mbolea nchini.


More Stories
Wafanyabiashara wahimizwa kutumia nembo ya Tanzania
Tozo ya mafuta yaboresha barabara Mwanza
Rungwe yaendelea kutatua changamoto za wakulima wa parachichi