October 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkurugenzi Bonde Rufiji, ahimiza utunzaji vyanzo vya maji

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbarali

WANANCHI wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wametakiwa kushiriki kikamilifu katika kutunza vyanzo vya maji na mazingira katika eneo la Usangu, ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa rasilimali hiyo.

Wito huo umetolewa Oktoba 3, 2026, na Mkurugenzi wa Maji wa Bonde la Rufiji, David Munkyala, wakati wa uzinduzi wa mashindano ya soka ya Rufiji Basin Cup wilayani Mbarali.

Mashindano hayo yameandaliwa na Taasisi Isiyo ya Kiserikali ya Save Life Organization of Tanzania (SALIOTA), kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira.

Munkyala amesema wakazi wengi wa Usangu wanategemea maji katika kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji mali, hivyo wanapaswa kushiriki katika uhifadhi wa rasilimali hiyo.

Amesisitiza pia umuhimu wa watumiaji wa maji kulipa ada kwa wakati, akieleza kuwa mapato hayo husaidia kugharamia shughuli za uhifadhi na usimamizi wa rasilimali za maji.

Amesema Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji inatekeleza mradi wa NBS Usangu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo LSF na SALIOTA.

Munkyala amesema mradi huo umehusisha pia mashindano ya soka yanayowakutanisha vijana kutoka vijiji 45, akiwataka washiriki kuzingatia haki, amani na utulivu.

Amesema endapo mashindano hayo yataendeshwa vizuri na kuonyesha matokeo chanya, kuna uwezekano wa kuongeza zawadi katika mashindano ya mwaka 2027.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa SALIOTA, Elisha Mwanikawaga, amesema mradi wa NBS Usangu unatekelezwa katika vijiji 45 kati ya 102 vya Mbarali, vilivyopo katika kata 16 kati ya 20 za wilaya hiyo.

Amesema kupitia michezo hiyo, wananchi wanahamasishwa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuacha ukataji miti ovyo, kutumia nishati safi na kutunza mazingira. Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Mariam Mnozya, amesema michezo ni njia muhimu ya kufikisha ujumbe wa uhifadhi wa mazingira kwa jamii.