May 6, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

MWADETA yahamasisha matumizi ya folic acid

Na Judith Ferdinand, Mwanza

IMEELEZWA kuwa ukosefu wa lishe bora, hasa madini ya folic acid, unachangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la watoto wanaozaliwa na kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Daktari Frank Munna wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania (MWADETA),amesema zaidi ya asilimia 95 ya visa hivyo vinatokana na upungufu wa lishe, si urithi kutoka kwa wazazi.

Akizungumza Mei 5,2026 wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHWs) 25 kutoka Wilaya ya Ilemela,juu ya vichwa vikubwa na mgongo wazi yalioandaliwa na taasisi na kufanyika wilayani humo,Dkt. Munna amesisitiza umuhimu wa matumizi ya folic acid miezi mitatu kabla ya ujauzito na ndani ya siku 28 za mwanzo za ujauzito.

Amesema,kipindi hicho ni muhimu kwa ukuaji wa mtoto, ambapo ukosefu wa madini hayo huongeza hatari ya mgongo wazi huku akisisitiza kuwa wahudumu hao wamewezeshwa kutoa elimu, kubaini mapema dalili za watoto wenye changamoto hizo ndani ya jamii na kuwa kuwasaidia kupata matibabu mapema na kufuatilia maendeleo yao.

“Dalili hizo ni pamoja na ukuaji usio wa kawaida wa kichwa, maumivu ya kichwa, matatizo ya kuona, kuzimia na degedege.Folic acid haitunzwi mwilini, hivyo ni muhimu kuitumia kila siku ili kulinda afya ya mama na mtoto kwa kuhakikisha matumizi ya vyakula vilivyorutubishwa kama unga wa mahindi wenye folic acid, pamoja na mboga za majani na matunda,”amesema Dkt.Frank.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za afya na uzazi na mtoto wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,Nyabwire Lukumai, amesema wanaendelea kuwasisitiza wahudumu hao kutoa elimu kwa wajawazito na wanaotarajia kubeba ujauzito kutumia dawa za folic acid ili kupungumza changamoto hizo.Amvapo dawa hizo katika vituo vya kutolea huduma za afya zinatolewa bure kwa mjamzito kila anapohudhuria kliniki za kutosha mwezi mzima.

“Tunawaelimisha wajawazito ajatambua umuhimu wa kutumia sawa hizo ambazo pia zinasaidia kuongeza damu kwa kumshauri muda sahihi,mfano akitumia asubuhi anapata hali ya kichefuchefu hivyo tunamshauri kutumia usiku baada ya kula akiwa anaenda kupumzika.Pia tunawatoa hofu kwani kuna wengine hawapendi kutumia folic acid wakidai wanapata haja kubwa nyeusi tunamueleza hiyo ni hali ya kawaida,”amesema Lukumai.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa MWADETA, Walter Miya,amesema Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando kwa mwaka inawaona watoto 700 hadi 800,tatizo ni kubwa kwani wapo ambao hawafiki wanabaki nyumbani au kupeleka kwa waganga wa kienyeji na wengine wanaishia kupoteza maisha wakiwa bado hawajapata matibabu.

“Hivyo tumeamua kutoa mafunzo wahudumu hao kwa wilaya nne za Mkoa wa Mwanza,awali tuluana na Nyamagana na kufikia 25, sasa ni Ilemela na baadae tutaenda Sengerema na Magu,lengo ni kuwapa elimu ya kufanya utambuzi wa awali ngazi ya jamii juu ya watoto wenye changamoto ya kichwa kikubwa, mgongo wazi na ulemavu mwingine ili kuwatambua mapema na kuweza kuwarufaa kwenda sehemu za matibabu mapema,”amesema Miya.

Naye Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Kata ya Buzuruga wilayani Ilemela,Abdul Mussa, amesema umaskini,imani za kidini na kimila ni moja ya changamoto zinazokwamisha jamii kupata matibabu,mfano unakuta mwanamke anaishi chini ya sheria za mwanaume hata kliniki anashindwa kuanza mapema anasubilia mpaka mume wake amwambie.

Hata hivyo Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Kata ya Pasiansi,Fungulia Fundikila, amesema kupitia elimu hiyo waliopata wataelimisha jamii,kuibua watoto wenye changamoto hizo pamoja na kuwaelekeza sehemu husika ya watoto hao kupata matibabu.