August 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jinsi Links Zinavyotumika Kwenye Wizi wa Mtandaoni

Mwandishi: Ismail Mayumba

Katika dunia ya kidijitali, “link” ni sehemu muhimu sana ya matumizi ya mtandao. Link ni maandishi au kifungo (button) ambacho ukikibonyeza kinakuhamisha kutoka sehemu moja kwenda nyingine inaweza kuwa tovuti, video ya YouTube, au kurasa za mitandao ya kijamii kama Instagram na Facebook. Urahisi huu wa kusafiri ndani ya mtandao bila kufunga programu moja na kufungua nyingine umeleta manufaa makubwa, lakini pia umefungua mlango kwa wahalifu wa mtandaoni.

Wahalifu hawa wamegundua kuwa watu wengi huamini links bila kuchunguza kwa kina, hivyo wanazitumia kama njia ya kuiba taarifa binafsi, akaunti, utambulisho, na hata fedha. Hii imefanya links kuwa moja ya mbinu kuu zinazotumika katika uhalifu wa mtandaoni.

Moja ya aina maarufu ya wizi ni ule wa kuiba akaunti, hasa akaunti za WhatsApp. Kwa mfano, watu hutumiwa links zinazodai kutoa misaada, nafasi za masomo (scholarships), au zawadi mbalimbali. Mtumiaji anapobonyeza link hiyo, anaombwa kuweka namba yake au kuthibitisha taarifa fulani. Hatua hiyo inaweza kusababisha akaunti yake kuchukuliwa na wahalifu. Ingawa wakati mwingine akaunti hurudishwa baada ya muda, kuna matukio mengi ambapo wahanga hupoteza akaunti zao kabisa. Mara nyingi, tatizo hili linachangiwa na tamaa ya kupata vitu vya bure au kwa urahisi.

Aina nyingine ni wizi wa taarifa binafsi. Hapa mtumiaji huingiza taarifa zake nyeti kama barua pepe (email), nenosiri (password), au taarifa za kifedha akidhani yuko kwenye mfumo salama. Taarifa hizi zinaweza kutumika kufanya uchambuzi wa tabia za watu, au hata kutumika vibaya dhidi ya jamii au taifa kwa ujumla. Hii inaonyesha kuwa madhara ya wizi wa mtandaoni hayamgusi mtu mmoja tu, bali yanaweza kuathiri jamii nzima.

Pia kuna mbinu ya kukupeleka kwenye tovuti za uongo (fake websites). Hapa wahalifu hutengeneza tovuti zinazofanana sana na zile halisi. Tofauti huwa ndogo sana kiasi kwamba ni vigumu kuitambua kwa haraka. Mfano, “islamicbank.com” inaweza kubadilishwa kidogo kuwa “1slamicbank.com”, ambapo herufi “I” inabadilishwa na namba “1”. Mtumiaji asipokuwa makini, anaweza kuingiza taarifa zake na kuishia kuibiwa fedha au data muhimu.

Mbinu nyingine ni ile inayojulikana kama “adware” au matangazo ya kulazimisha. Unapofungua tovuti fulani, unaweza kubonyeza sehemu moja tu na ghafla ukapelekwa kwenye ukurasa mwingine usiotarajia. Mara nyingi kurasa hizi huhusiana na kamari, maudhui yasiyofaa, au biashara haramu. Tatizo hili huwapata sana watu wanaopenda huduma za bure zisizo rasmi, kama kuangalia mechi au filamu bila kulipia.

Ili kujilinda dhidi ya hatari hizi, ni muhimu kuchukua tahadhari zifuatazo:
Kwanza, epuka kubonyeza links kutoka kwa watu usiowafahamu au ujumbe usioeleweka, hasa kwenye makundi ya mitandao ya kijamii. Pili, jiepushe na tovuti zinazotoa huduma za bure kwa njia zisizo halali. Tatu, hakikisha unachunguza link kabla ya kuifungua, na kama una shaka, uliza kwa mtu mwenye uelewa wa teknolojia.

Ni muhimu pia kufahamu kuwa zamani watu waliamini kuwa link yenye “HTTP” si salama na ile yenye “HTTPS” ni salama. Hata hivyo, siku hizi wahalifu wanatumia pia “HTTPS”, hivyo uwepo wa alama hiyo pekee hauhakikishi usalama. Mtumiaji anapaswa kuchunguza zaidi uhalali wa tovuti kabla ya kuamini.

Kwa ujumla, links ni sehemu ya kawaida ya maisha ya mtandaoni, lakini pia ni silaha inayoweza kutumiwa vibaya. Elimu na umakini ni kinga muhimu zaidi dhidi ya wizi wa mtandaoni.