
Na Joyce Kasiki
WAKATI Dunia ikiendelea kukitambua Kiswahili kama lugha inayokua kwa kasi kimataifa, macho ya wadau wa lugha hiyo yanaelekezwa jijini Paris, Ufaransa, kuanzia Julai 4 hadi 7 mwaka huu.
Hapo ndipo linapofanyika Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili sambamba na maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, tukio linalotarajiwa kuibua fursa mpya za lugha hiyo katika elimu, biashara, teknolojia na diplomasia.
Kongamano hilo linawakutanisha wataalamu wa lugha, wanataaluma, viongozi wa serikali, wanadiplomasia, wafanyabiashara, waandishi pamoja na wadau wengine kutoka mataifa mbalimbali kujadili nafasi ya Kiswahili katika elimu, biashara, teknolojia, utamaduni na diplomasia.
Kwa Tanzania, Taifa linalotambulika kama kitovu cha maendeleo ya Kiswahili cha kisasa, kongamano hilo ni zaidi ya mkutano wa kitaaluma. Ni jukwaa la kimkakati linaloweza kufungua milango ya fursa za kiuchumi, kielimu na kidiplomasia huku likiiweka nchi katika nafasi ya kunufaika zaidi na ukuaji wa lugha hiyo duniani.
Kadiri vyuo vikuu na taasisi mbalimbali duniani zinavyoendelea kuanzisha programu za kufundisha Kiswahili, ndivyo mahitaji ya walimu, wakalimani, watafiti, waandishi wa vitabu, wachapishaji na wataalamu wa teknolojia za lugha yanavyozidi kuongezeka. Hali hiyo inaifanya Kiswahili kuwa rasilimali ya maendeleo badala ya kuwa lugha ya mawasiliano pekee.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Consolata Mushi, anasema Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kunufaika na ongezeko la matumizi ya Kiswahili duniani kupitia sekta za elimu, tafsiri, teknolojia za lugha, utalii wa utamaduni, sanaa, vyombo vya habari na maudhui ya kidijiti.
Anasema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Kubidhaisha Kiswahili wa miaka 10 uliozinduliwa mwaka 2022, unaolenga kukuza taaluma za Kiswahili, kuimarisha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia lugha hiyo, kuongeza machapisho ya Kiswahili pamoja na kupanua huduma za tafsiri, ukalimani, uhariri, ufundishaji na utangazaji.
Kwa mujibu wa Mushi, utekelezaji wa mkakati huo umeendelea kufungua ajira kwa walimu, watafiti, waandishi, wataalamu wa lugha na vijana wenye ubunifu katika teknolojia za kisasa.
Mafanikio ya Kongamano la Kwanza la Kimataifa la Kiswahili lililofanyika Havana, Cuba mwaka 2024 yanaonyesha wazi kuwa Kiswahili kinaendelea kuvuka mipaka.
Kupitia kongamano hilo, matumizi ya Kiswahili katika nchi zinazozungumza Kihispania yaliongezeka, huku Chuo Kikuu cha Havana kikianzisha mafunzo ya Kiswahili kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Vitabu, kamusi na machapisho yaliyoandaliwa nchini Tanzania sasa yanatumika kufundishia Kiswahili katika taasisi mbalimbali za elimu duniani. Hii ni ishara kwamba lugha hiyo imeanza kuwa bidhaa yenye thamani ya kiuchumi inayoweza kuingizia taifa mapato kupitia elimu na huduma za lugha.
Mbali na elimu, Kiswahili kimeendelea kuwa mhimili wa uchumi wa ubunifu.
Filamu, muziki, tamthilia, vitabu, michezo ya kidijiti na maudhui ya mtandaoni yanayotumia Kiswahili yanaendelea kupata soko kubwa duniani, jambo linaloongeza mapato kwa wabunifu na kuitangaza Tanzania kimataifa.
Katika diplomasia, Kiswahili sasa ni lugha rasmi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), Umoja wa Afrika (AU), UNESCO na taasisi nyingine za kimataifa.
Hadhi hiyo inaifanya Tanzania kuwa na wajibu mkubwa wa kuendelea kuongoza juhudi za kuikuza lugha hiyo duniani.
Mbunge wa Kakonko, Allan Mvano, ameipongeza Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuendelea kuikuza na kuitangaza Kiswahili katika jukwaa la kimataifa.
Ametoa wito kwa wajumbe wote watakaoshiriki kongamano hilo kuwa mabalozi wa Kiswahili kwa kuitangaza lugha hiyo kama urithi muhimu wa Afrika na nyenzo ya maendeleo.
Pia ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na balozi za Tanzania zilizopo katika nchi mbalimbali kutumia Kiswahili kama nyenzo ya kutangaza fursa za uwekezaji, biashara na utalii zilizopo nchini.
“Watanzania tuna kila sababu ya kueneza Kiswahili duniani kwani lugha hii inaweza kufungua milango ya ajira, biashara na ushirikiano wa kimataifa,” amesema Mvano.
Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema Kiswahili kina historia kubwa barani Afrika na duniani, huku takribani watu milioni 500 wakikitumia kwa viwango tofauti.
Amesema uwepo wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kongamano hilo kama mgeni rasmi utakuwa fursa muhimu ya kuiambia dunia kuwa Kiswahili si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni chombo cha umoja, maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Christina Mzava, amesema kongamano la Paris litayavutia mataifa mengi zaidi kuanza kujifunza Kiswahili, jambo litakaloongeza mahitaji ya wataalamu wa lugha hiyo pamoja na kufungua fursa mpya za biashara.
Ameeleza kuwa kadiri wageni wengi wanavyojifunza Kiswahili, ndivyo watakavyovutiwa kuja Tanzania kufanya biashara, kuwekeza na kutembelea vivutio vya utalii, huku Watanzania nao wakipata nafasi kubwa ya kufanya biashara katika masoko ya kimataifa.
Ni wazi kwamba Kongamano la Pili la Kimataifa la Kiswahili si tukio la lugha pekee, bali ni jukwaa la maendeleo. Ikiwa Tanzania itaendelea kuwekeza katika elimu ya Kiswahili, teknolojia, tafsiri, ubunifu na diplomasia ya lugha, itaweza kuigeuza hazina hiyo kuwa chanzo kikubwa cha ajira, mapato na ushawishi wa kimataifa.
Paris inaweza kuwa hatua nyingine kubwa ya safari ya Kiswahili kuelekea kuwa lugha yenye nguvu zaidi duniani, lakini mafanikio yake yatategemea namna ambavyo Tanzania na wadau wake watatumia fursa hiyo kuigeuza lugha kuwa mtaji wa maendeleo endelevu.

More Stories
Walipakodi wahimizwa kutumia usuluhishi kutatua migogoro ya kodi
Watatu mbaroni tuhuma mauaji ya bibi yao
UDSM yaongeza thamani ulanzi kupitia utafiti bunifu nchini