July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu mbaroni tuhuma mauaji ya bibi yao

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online, Mbeya

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu watatu wanaodaiwa kumuua bibi yao, Mary Mwasile (70), mkazi wa Kijiji cha Isongole, Wilaya ya Mbeya, katika tukio linalohusishwa na imani za ushirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Yella Mboya (27), mkazi wa Tunduma mkoani Songwe, Furaha Mboya (25) na Elisa Mboma (43), wote wakazi wa Kijiji cha Isongole.

Akizungumza na waandishi wa habari Julai 3,2026, Kamanda Kuzaga alisema tukio hilo lilitokea Juni 28, 2026, majira ya saa nne asubuhi katika Kijiji cha Isongole, Kata ya Santilya, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya, ambapo mwili wa marehemu ulikutwa ndani ya nyumba yake ukiwa na jeraha la kuchomwa shingoni kwa kitu chenye ncha kali.

Amesema baada ya tukio hilo, Jeshi la Polisi kupitia kikosi maalumu cha kuzuia na kupambana na matukio ya mauaji kilianzisha uchunguzi na msako uliowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao.

“Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha mauaji hayo ni imani za kishirikina. Uchunguzi unaendelea ili kubaini mazingira yote ya tukio na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa,” amesema Kamanda Kuzaga.

Katika tukio jingine, Kamanda Kuzaga alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) linawashikilia Shughuli Halezya (50), Shabani Matulu (36) na Baraka Mwaluswaswa (26), wote wakazi wa Lualaje, Wilaya ya Chunya, kwa tuhuma za kukutwa na silaha aina ya gobole bila kibali.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa Juni 30, 2026, wakati wa msako uliofanyika katika Kijiji cha Bitimanyanga, Kata ya Mafyeko, Wilaya ya Chunya.

Kamanda Kuzaga amesema kuwa katika mwezi Juni 2026, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwakamata jumla ya watuhumiwa 239 wanaohusishwa na makosa mbalimbali ya jinai, yakiwemo mauaji, kujeruhi, ubakaji, umiliki haramu wa silaha na matukio ya wizi.

Ameongeza kuwa baadhi ya watuhumiwa tayari wamefikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa kesi zao kukamilika, huku uchunguzi wa kesi zilizobaki ukiendelea.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuachana na imani potofu za ushirikina na badala yake kutumia vyombo vya dola kutatua migogoro au kutoa taarifa za vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.