July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

UDSM yaongeza thamani ulanzi kupitia utafiti bunifu nchini

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online

CHUO Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM),kimefanya utafiti uliozalisha bidhaa mbalimbali zinazotokana na ulanzi, hatua inayolenga kuongeza thamani ya zao hilo, kulihifadhi dhidi ya kutoweka na kuongeza kipato cha wakulima wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Akizungumza Julai 3, 2026, na waandishi wa habari katika banda la UDSM kwenye Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE), Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dkt. Lewis Mtashobya alisema ulanzi ni zao la asili linalopatikana zaidi katika mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Songwe na Rukwa, lakini limekuwa katika hatari ya kupotea kutokana na kushuka kwa thamani yake na kutegemea matumizi ya kutengeneza kinywaji cha kilevi pekee.

Alisema wakati wa msimu wa mvua ulanzi unapokuwa mwingi, bei yake hushuka hadi Sh2,000 kwa ujazo wa mita moja, huku kipindi cha kiangazi ukifikia kati ya Sh9,000 na Sh10,000, jambo linalowakatisha tamaa wakulima kuendelea kulima zao hilo.

“Baadhi ya wananchi pia wameacha kujihusisha na ulanzi kutokana na sababu za imani za dini, kwani walikuwa wakilitumia zaidi kutengeneza pombe. Hali hiyo imesababisha miti mingi kuachwa na kuanza kupotea,” alisema.

Dkt. Mtashobya alisema watafiti wa UDSM wameamua kubuni matumizi mbadala ya ulanzi kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali zisizo za kilevi ili kuongeza soko na thamani ya zao hilo.

Alitaja baadhi ya bidhaa zilizotengenezwa kuwa ni vimiminika vya maabara na hospitali kwa ajili ya kuhifadhi sampuli za viumbe hai, dawa za kusafishia na kutunzia vifaa vya maabara pamoja na bidhaa nyingine zinazoweza kutumika katika sekta ya elimu, afya na viwanda.

Alifafanua kuwa bidhaa hizo zimeonyesha uwezo mkubwa wa kuhifadhi viumbe kwa muda mrefu bila kuoza, hivyo kupunguza gharama za upatikanaji wa vifaa vya kufundishia katika shule, vyuo na maabara.

Aidha, alisema mabaki yanayobaki baada ya uchakataji wa ulanzi pia yanatumika kuzalisha bidhaa nyingine, hatua inayosaidia kutumia malighafi yote bila kupoteza sehemu yoyote ya zao hilo.

Dkt.Mtashobya alisema lengo la utafiti huo ni kuifanya kilimo cha ulanzi kiwe cha kibiashara, kuongeza ajira, kuinua kipato cha wakulima na kuhifadhi zao hilo la asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Alitoa wito kwa wananchi, wawekezaji na wadau mbalimbali kutembelea banda la UDSM katika Maonyesho ya Sabasaba ili kujionea bidhaa hizo za ubunifu na kupata elimu kuhusu fursa zilizopo katika kuongeza thamani ya mazao ya asili kupitia utafiti na teknolojia.