August 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yaongeza kasi kuchochea uchumi wa buluu Zanzibar

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, imeongeza kasi ya uwekezaji katika miundombinu na huduma za kidijitali Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuunga mkono ukuaji wa uchumi wa buluu na sekta ya utalii visiwani humo.

Uwekezaji huo unahusisha upanuzi na uboreshaji wa mtandao katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba, hususan maeneo yenye shughuli kubwa za utalii na biashara, ili kuongeza upatikanaji wa intaneti yenye kasi na uhakika kwa wananchi, wafanyabiashara na wageni wanaotembelea Zanzibar.

Akizungumza wakati wa Tamasha la Kizimkazi, lililofanyika hivi kaeibuni, Mkuu wa Yas Zanzibar, Mohamed Waqid amesema ukuaji wa sekta ya utalii umeongeza mahitaji ya huduma bora za mawasiliano, huku matumizi ya teknolojia yakizidi kuwa sehemu muhimu katika uendeshaji wa shughuli za sekta hiyo.

Amesema, kutokana na hali hiyo, Yas imeendelea kuimarisha mtandao wake katika maeneo ya utalii ili kuhakikisha wakazi wa Zanzibar, wageni na wafanyabiashara wanapata huduma za mawasiliano zinazokidhi mahitaji yao.

“Katika kuunga mkono sekta ya utalii, tumeendelea kuwekeza katika mtandao wenye kasi na uhakika kwenye maeneo mbalimbali.

*Tunataka kuhakikisha wakazi wa Zanzibar na vilevile wageni wanapofika Zanzibar waweze kuwasiliana na familia zao na kupata huduma za kidijitali kwa urahisi, lakini pia wadau wa utalii waweze kutumia mtandao wetu kuendesha shughuli zao,” amesema Waqid.

Ametaja maoneo mbalimbali kama; Kizimkazi, Makunduchi, Paje, Jambiani na Michamvi kuwa miongoni mwa maeneo ambayo Yas imeendelea kuimarisha huduma za mtandao kutokana na kukua kwa shughuli za utalii, biashara na uwekezaji.

Kwa mujibu wa Waqid, uwepo wa mtandao wa uhakika katika maeneo hayo unatoa fursa kwa hoteli, migahawa, waongoza watalii, watoa huduma za usafiri na wajasiriamali wengine kutumia teknolojia kuwasiliana na wateja, kutangaza huduma zao na kuyafikia masoko mapya.

Mbali na kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano, alisema Yas imeendelea kuwezesha upatikanaji wa simu janja, ikiwa ni njia ya kuwawezesha wananchi, hususan vijana na wajasiriamali, kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

“Tunawawezesha pia wajasiriamali kupata simu janja ili waweze kuingia katika ulimwengu wa kidijitali. Leo teknolojia inatoa fursa nyingi za kukuza biashara, kupata taarifa na kufikia wateja wapya, hivyo tunataka vijana wetu wawe sehemu ya fursa hizo,” amesema.

Tamasha la Kizimkazi limekuwa likiwakutanisha wakazi wa Zanzibar, wageni kutoka Tanzania Bara na nje ya nchi, huku likitoa nafasi ya kuonesha utamaduni wa Kizanzibari, kutangaza vivutio vya utalii na kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wake, Issa Juma Nahoda, mwalimu na mkazi wa Makunduchi, ambaye alitembelea banda la Yas wakati wa tamasha hilo na kununua rauta ya 5G kwa matumizi ya nyumbani, amesema intaneti ya uhakika imekuwa hitaji muhimu kutokana na shughuli nyingi za kazi na elimu kutegemea mifumo ya kidijitali.

Yas imesema, itaendelea kupanua na kuboresha miundombinu yake ya mawasiliano Zanzibar ili kwenda sambamba na ongezeko la mahitaji ya huduma za kidijitali na kuchangia maendeleo ya sekta za utalii, biashara na ujasiriamali, ambazo zina nafasi muhimu katika ukuaji wa uchumi wa buluu visiwani humo.