Na Joyce Kasiki, Timesmajiraonline, Tanga
WAFUGAJI sasa wanaweza kutumia teknolojia kufuatilia mwenendo wa mifugo yao, kutunza historia za huduma za afya na kupata taarifa za msingi za uzalishaji kupitia mfumo wa Mnyama Check App unaotolewa na kampuni ya Afya Nyama Digital.
Mfumo huo ni bunifu iliyoundwa kwa kutumia vifaa vinavyofungwa kwa wanyama na kuhusishwa na mfumo wa kidijitali, hali inayomwezesha mfugaji kupata taarifa mbalimbali zinazohusu mifugo yake bila kutegemea ufuatiliaji wa kawaida pekee.
Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Afya Nyama Digital, Maganga Mabula, akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Elimu,Ujuzi na Ubunifu yanayoendelea katika viwanja vya Usagara jijini Tanga alisema ubunifu huo unalenga kuwasaidia wafugaji kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa badala ya kusubiri changamoto za mifugo kujitokeza.
Mabula amesema miongoni mwa taarifa zinazoweza kufuatiliwa ni mabadiliko yanayohusiana na afya ya mnyama, hali ya uzazi na vipindi muhimu vinavyohitaji uangalizi wa mfugaji.
Amesema,Mfumo huo pia umewekewa sehemu ya kuhifadhi historia ya kila mnyama, ikiwamo taarifa za chanjo na matibabu yaliyowahi kutolewa. Taarifa hizo zinaweza kumsaidia mfugaji kufuatilia huduma zilizotolewa na kujua hatua zinazofuata.
Mbali na afya amesema ,teknolojia hiyo inahusisha taarifa za uzalishaji na mauzo,mfugaji anapokuwa tayari kuuza mnyama, anaweza kutumia taarifa zilizohifadhiwa kuonyesha historia yake kwa mnunuzi, jambo linaloweza kuongeza uwazi katika biashara ya mifugo.
Mabula alisema huduma hiyo pia imejumuisha mfumo wa kuwaunganisha wafugaji na wataalamu wa mifugo, huku kampuni ikishirikiana na madaktari na wataalamu hao katika ufungaji wa vifaa na utoaji wa maelekezo kwa watumiaji.
Kwa wafanyabiashara wanaohusika na huduma za mifugo amesema ,mfumo unaweza kutumika katika uendeshaji wa shughuli zao, ikiwamo kufuatilia bidhaa na taarifa za biashara.
Amesema,huduma za Mnyama Check zinapatikana kupitia majukwaa ya simu pamoja na tovuti ya kampuni na kwamba watumiaji wanaweza kujisajili na kupata huduma zinazohusiana na mfumo, ikiwamo upatikanaji wa vifaa kupitia Mnyama Shop.
Mabula amesema,kampuni imekuwa ikishirikiana na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) katika kuendeleza ubunifu huo huku akisema ushirikiano huo umechangia katika kuongeza uwezo wa kampuni katika maeneo ya teknolojia na ukusanyaji wa taarifa.
Amesema msaada huo pia umeifanya kampuni iweze kuwasilisha ubunifu wake kwa wadau kwa ufanisi zaidi na kujenga mazingira ya kuaminika kwa wateja na mashamba yanayotumia huduma zake.
Kampuni hiyo imewataka wadau wa sekta ya mifugo kuendelea kutumia teknolojia katika shughuli zao, hasa katika kipindi ambacho taarifa sahihi na zinazopatikana kwa wakati zina umuhimu katika kuongeza ufanisi wa ufugaji.
Mfugaji kutoka Pwani Sarafia Kamwela mnufaika wa Mfumo huo amesema matumizi ya mfumo huo yameongeza uelewa wake kuhusu afya ya mifugo, ikiwemo uwezo wa kutambua dalili za awali za magonjwa na kuchukua hatua kwa wakati. Kwa mujibu wake, upatikanaji wa ushauri wa kitaalamu kwa njia ya teknolojia umepunguza changamoto ya kusubiri daktari wa mifugo kufika eneo alipo, jambo linalomsaidia kuzuia madhara makubwa kwa mifugo.
Amesema kabla ya kutumia mfumo huo, baadhi ya changamoto za kiafya za mifugo zilikuwa zikimlazimu kutafuta msaada kutoka kwa wataalamu kwa njia za kawaida, hali ambayo wakati mwingine ilichukua muda. Hata hivyo, matumizi ya mfumo huo yamemwezesha kupata mwongozo wa kitaalamu kwa urahisi zaidi na kumsaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu hatua za kuchukua.
Kwa sasa, amesema anaendelea kuhamasisha wafugaji wenzake kutumia teknolojia katika shughuli zao za kila siku, akisisitiza kuwa mabadiliko ya kiteknolojia yanaweza kuwa chachu ya kuongeza tija, kupunguza hasara na kuboresha ustawi wa mifugo.

More Stories
wanawake magereza wahimizwa kujenga uwezo , kutumia fursa kidijitali
Aweso amrejesha Mha.Msenyele kuongaza MWAUWASA
GBT yawataka wachezaji kucheza kwa kiasi