Na Joyce Kasiki, Tanga
SERIKALI imesisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika sayansi, teknolojia, na ubunifu ili kuongeza kasi ya maendeleo ya Tanzania na kuiwezesha nchi kutimiza malengo yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Hayo yamesemwa leonAgosti 16,2026 na Mkurugenzi wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ladislaus Mnyone wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, ambako yanaendelea Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu.
Prof. Mnyone amesema maadhimisho hayo, yameanza Agosti 15 hadi 24, 2026, yanalenga kuwakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kuendeleza elimu, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu kwa manufaa ya Taifa.
Aidha amesema maadhimisho hayo yatazinduliwa Agosti 18,2026 na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla
Amesema maadhimisho hayo pia yanatoa fursa kwa wananchi kujionea teknolojia na bunifu mbalimbali zinazolenga kutatua changamoto katika sekta tofauti, ikiwemo kilimo, mifugo, maji, madini na maeneo mengine ya uzalishaji.
“Usidhani unapokuja hapa unaona teknolojia za elimu pekee. Sayansi na teknolojia zinahusu sekta zote, hivyo tutaona teknolojia katika kilimo, mifugo, maji, madini na sekta nyingine,” amesema Prof. Mnyone
Amesema Tanzania inapotekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inapaswa kuongeza uwezo wa kuzalisha na kutumia teknolojia zinazobuniwa nchini ili kupunguza utegemezi wa teknolojia kutoka nje.
Kwa mujibu wa Prof. Mnyone, miongoni mwa matarajio ya Dira ya 2050 ni Tanzania kujenga uchumi wenye thamani kubwa, kuongeza kipato cha mwananchi na kuhakikisha Watanzania wengi wanapata ajira zenye staha.
Amesema ili kufikia malengo hayo, Serikali na wadau wengine wanapaswa kuongeza uwekezaji katika sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu, akieleza kuwa uwekezaji huo una uwezo wa kuongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Endapo tutaendelea kubaki tegemezi kwa kiasi kikubwa katika teknolojia kutoka nje, uwezo wetu wa kufikia matarajio ya Dira ya 2050 unaweza kuwa mgumu. Tunahitaji kuongeza uwezo wa kuzalisha na kutumia teknolojia ndani ya nchi,” amesema.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha tafiti zinazolenga kutatua changamoto zinazowakabili wananchi katika sekta mbalimbali, akisema utafiti unaozingatia mahitaji halisi ya jamii unaweza kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo.
Prof. Mnyone amesema baadhi ya mataifa yaliyowekeza kwa nguvu katika sayansi na teknolojia yamepiga hatua kubwa kiuchumi, hivyo Tanzania inapaswa kujifunza kutoka kwa mataifa hayo na kuongeza juhudi katika maeneo hayo.
Amesema dhana ya sayansi, teknolojia na ubunifu haipaswi kuhusishwa na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pekee, bali inahusisha maeneo mapana yanayogusa maisha na shughuli za kiuchumi na kijamii.
“TEHAMA ni sehemu ndogo tu ya sayansi, teknolojia na ubunifu. Dhana hii ni pana na inagusa kila sekta na kila eneo la jamii,” amesema
.
Kwa upande mwingine, Prof. Mnyone amesema mafanikio katika sayansi, teknolojia na ubunifu yanahitaji rasilimali watu wenye maarifa na ujuzi unaokidhi mahitaji ya wakati, hivyo Serikali itaendelea kuimarisha mafunzo ya wataalamu katika maeneo hayo.
Amesema maadhimisho hayo pia yanalenga kutoa nafasi kwa wadau kujadili namna elimu na ujuzi vinavyoweza kuunganishwa na sayansi, teknolojia, utafiti na ubunifu ili kuzalisha wataalamu watakaoweza kuchochea maendeleo ya Taifa.
Maadhimisho hayo yanatarajiwa kufikia kilele Agosti 24, 2026, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya Prof. Mnyone, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya kufunga maadhimisho hayo.

More Stories
Yas yaongeza kasi kuchochea uchumi wa buluu Zanzibar
Prof.Mnyone apongeza ubunifu VETA kusaidia wananchi
TANTRADE yashiriki hafla ya ufungaji wa maonesho ya 10 ya Wakulima Zanzibar