August 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Prof.Mnyone apongeza ubunifu VETA kusaidia wananchi



Na Joyce Kasiki, Tanga


MKURUGENZI wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026, Profesa Ladislaus Mnyone, amepongeza ubunifu unaooneshwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), akisema teknolojia hizo zina uwezo wa kuwasaidia wananchi kuongeza kipato na kuchangia uchumi wa Taifa.


Profesa Mnyone amesema hayo leo Agosti 16,2026 alipotembelea banda la VETA katika viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Usagara jijini Tanga, ambako yanafanyika maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026.


Amesema ameridhishwa na ubunifu aliouona katika banda hilo kwa kuwa baadhi ya teknolojia zimebuniwa kwa kuzingatia mahitaji na changamoto zinazowakabili wananchi wa kawaida, hususan wanaojishughulisha na kilimo, ufugaji na shughuli nyingine za uzalishaji.


Ametolea mfano mashine ya kuhifadhia matunda na mashine (incubator) ya kutotolesha vifaranga, akisema teknolojia hizo zinaweza kutumiwa na wananchi kuongeza thamani ya shughuli zao za kiuchumi.


“Nimeona teknolojia ya jokofu la kuhifadhia matunda ambalo mwananchi wa kawaida anaweza kulitumia kuhakikisha matunda yake yanahifadhiwa vizuri akisubiri soko na kuyauza yakiwa bado katika hali nzuri,” amesema Profesa Mnyone.


Amesema pia incubator ya kutotolesha vifaranga inayooneshwa na VETA ni teknolojia rahisi ambayo inaweza kutumiwa na wananchi kuzalisha vifaranga na kujipatia kipato.


Kwa mujibu wa Profesa Mnyone, kuendelezwa na kuenezwa kwa teknolojia hizo kutasaidia kuongeza tija kwa wananchi na hatimaye kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.


Amesisitiza umuhimu wa Serikali na wadau kuendelea kuweka mazingira mazuri ya kukuza, kuendeleza na kufanya teknolojia zinazobuniwa nchini zitumike kibiashara, ili Tanzania iwe soko kubwa la teknolojia na bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi.


Kwa upande wake, Meneja wa Uhusiano wa VETA, Sita Peter, amesema taasisi hiyo inatumia maadhimisho hayo kuwaonesha wananchi namna inavyotoa mchango katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 kupitia elimu, ujuzi na ubunifu.


Amesema VETA inaonesha programu mbalimbali za mafunzo na ubunifu zinazolenga kujenga uchumi imara, shindani na shirikishi, sambamba na kuwaandaa vijana wenye maarifa na ujuzi wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.


Peter amesema VETA imeanza programu mpya za mafunzo katika sekta ya madini, ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu zinazochangia uchumi wa nchi.


Amesema programu hizo zinahusisha maeneo sita ya mafunzo yanayolenga kuongeza ujuzi na tija katika shughuli za madini, huku wananchi wakipewa fursa ya kupata taarifa kuhusu fursa za mafunzo katika maeneo hayo.


Aidha, amesema VETA inaandaa mazingira ya kuwawezesha wanafunzi kupata sifa za kitaaluma zinazotambulika kimataifa, ikiwemo kuandaa vifaa na miundombinu katika vyuo vyake ili kuboresha utoaji wa mafunzo hayo.


Peter amesema VETA pia inatekeleza mradi wa ESPJ unaolenga kuongeza fursa za elimu na ujuzi kwa ajira zenye tija, huku ikilenga kuwaandaa vijana wanaohitimu mafunzo kuwa na uwezo wa kujiajiri na kutengeneza ajira.


Katika eneo la utunzaji wa mazingira, amesema VETA imepanda jumla ya miti 130,800 katika vyuo vyake, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuchangia katika kukabiliana na changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.


Amesema pia vyuo 26 vya VETA vimeunganishwa na matumizi ya nishati safi, ikiwemo gesi na nishati mbadala ya mkaa.


Ameongeza kuwa Chuo cha VETA Moshi kinaendelea kuimarisha ubunifu wa majiko rafiki kwa mazingira yanayotumia mkaa mbadala, hatua inayolenga kupunguza athari za matumizi ya nishati zisizo rafiki kwa mazingira.