July 4, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Walipakodi wahimizwa kutumia usuluhishi kutatua migogoro ya kodi

Na Mwandishi Wetu,Timesmajira

OFISI ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi imewahimiza walipakodi na wadau wa kodi kutumia huduma za usuluhishi katika kutatua migogoro ya kikodi kwa wakati, hatua inayosaidia kuimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na kuongeza ulipaji wa kodi kwa hiari.

Akizungumza Julai 2, 2026 katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba), Msuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi, Erastus Mtui, alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu haki zao za kikodi, majukumu ya ofisi hiyo pamoja na kupokea na kushughulikia malalamiko yanayohusiana na kodi.

Alisema ofisi hiyo ilianzishwa ili kutoa jukwaa huru kwa wafanyabiashara, wawekezaji na walipakodi wengine kuwasilisha changamoto zao za kikodi na kupata suluhu kwa haraka, jambo linalochangia kuondoa vikwazo vinavyoweza kuathiri shughuli za biashara na uwekezaji.

“Ulipaji wa kodi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa. Hivyo, tunahakikisha changamoto zinazowakabili walipakodi zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati ili zisikwamishe utekelezaji wa wajibu wao wa kulipa kodi,” alisema Mtui.

Aliongeza kuwa shughuli za ofisi hiyo zinaunga mkono utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi shindani unaotegemea mazingira bora ya biashara, uwekezaji na ongezeko la mapato ya ndani.

Kwa mujibu wa Mtui, wananchi wanaweza kuwasilisha malalamiko yao kupitia ofisi za taasisi hiyo, simu za bure, mfumo wa mtandao pamoja na programu ya Suluhu ya Kodi App. Aidha, alisema maandalizi ya mfumo wa USSD yanaendelea kukamilishwa ili kuwezesha huduma kuwafikia hata watumiaji wa simu zisizo janja.

Alisema tangu kuanzishwa kwa ofisi hiyo takribani miaka miwili na nusu iliyopita, jumla ya malalamiko 593 yamepokelewa na kushughulikiwa, huku malalamiko 340 yakitatuliwa katika mwaka uliopita pekee.

Mtui aliwataka wananchi, wafanyabiashara na wadau wengine wa kodi kutembelea banda la Ofisi ya Usuluhishi wa Malalamiko na Taarifa za Kodi katika Maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu zaidi kuhusu huduma zinazotolewa na njia mbalimbali za kuwasilisha malalamiko ya kikodi.