April 29, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwendo wa Rais Samia kalamu tu, sio kufoka

Na Mwandishi Wetu,TimesmajiraOnline,Dar

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameendelea kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali na kubadilisha wengine kwenye nafasi zao, hali inayoonesha wazi kwamba anataka viongozi wakaowaletea Watanzania matokeo.

Aidha, uamuzi huo wa Rais Samia umetafsiriwa kuwa ni mwendelezo wa falsafa yake ya kufoka kwa kalamu pale ambapo wateule wake wanashindwa kuendana na makudio yake.

Hiyo inadhihirishwa na teuzi alizozifanya kuanzia mwezi huu zingine zikiwa zimetangazwa usiku wa kuamkia leo.

Kama ilivyo kawaida yake mkeka wa viongozi walioteliwa na kuhamishwa vituo vyao vya kazi ulitolewa usiku na
na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Huko nyuma, Rais Samia aliwahi kuwatahadharisha wateule wake kwamba, “Msinitegemee kwa maumbile yangu haya, pengine na malezi yangu kukaa hapa na kufoka.

Nahisi si heshima, nafanya kazi na watu wazima wanaojua jema na baya na kila mtu anajua afanye nini, msitegemee nitaanza kufoka hovyo hovyo, nitafoka kwa kalamu,” Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alirudia kauli kama hiyo wakati wa kuapisha viongozi mbalimbali Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma Aprili 2, 2022, ambapo alisisitiza kwamba kamwe haitatokea afoke na hata siku za nyuma alishawahi kusema hivyo, kwa kuwa yeye ni mama mlezi.

“Huko nyuma nilisema sitafoka, nitafanyakazi ka kalamu, nitawakumbusha, lakini sitafoka, hata ukitazama sijaumbwa kufokafoka na mimi ni mama, ni mlezi, nitajaribu kuwalea, lakini ulezi utakaponishinda nitachukua hatua kali,” alisema Rais Samia.

Alisema bado ana kazi kubwa ya kuwaelimisha watumishi wa umma kuhusu dhana ya ukuaji kitaifa, ili waondokana na dhana ya ukuaji binafsi.

“Tunapozungumzia growth watu hawana picha kwamba ukuaji tunaozungumza ni wa nchi kwa ujumla, kuna watu wanajitazama kwa ujumla, niko hapa nakuaje, natokaje, nakaa miaka mingapi na natoka na nani.

Hatuviziani, wajibu wangu ni kukuza uchumi, kuleta uimara wa Taifa langu,” alisema. Wachambuzi wanasema kwamba mabadiliko anayofanya Rais Samia ni kielelezo kwamba wapo wateule wake hawatimizi majuku yao kama ilivyokusudia, ndiyo maana anazidi kufoka kwa kalamu.

Joseph Peter, mkazi wa Dar es Salaam amesema yaliyoibuliwa kwenye ziara za chama zilizofanywa na Paul Makondo, ni miongoni mwa mambo ambayo yanaonesha kushindwa kuwajibika baadhi ya wateule wa Rais.

“Kama baadhi ya wateule wa Rais wangefanyakazi zao ipasavyo, tuliyoyaona kwenye mikutano ya Makonda yasingekuwa kwa kiwango kile, unakuta mkuu wa mkoa yupo, DC yupo, DED yupo, lakini wanashindwa kusaidia wananchi, hii haikubaliki, namuunga mkono Rais,” alisema.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa usiku wa kuamkia jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus, Rais Samia, alimteua, Anamringi Macha kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kabla ya uteuzi huo, Macha alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM). Aidha, amemteua Christina Mndeme kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Kabla ya uteuzi, Mndeme alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga. Pia amemteua Japahari Mghamba kuwa Mkuu wa Wilaya ya Lushoto. Kabla ya uteuzi huu, Mghamba alikuwa Katibu Tawala wa
Wilaya ya Busega.

Katika uteunzi mwingine, Rais Samia amemteua, Mussa Kilakala kuwa Mkuu wa Wilaya ya Pangani. Kabla ya uteuzi huu, Kilakala alikuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Kaliua.

Aidha, alimteua Robert Masunya kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa. Kabla ya uteuzi huu, Masunya alikuwa Afisa Mwandamizi katika Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.

Pia alimteua, Mwashabani Mrope kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Mji wa Korogwe. Alimteua, Jacob Nkwera kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba. Kabla ya uteuzi huu, Nkwera alikuwa Afisa Mwandamizi, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Mwingine aliyemteua Rais Samia ni Sangai Mambai kuwa Katibu Tawala wa Wilaya ya Busega, huku akimteua akimteua Raymond Mweli kuwa Katibu tawala wa Wilaya ya Kaliua.

Wakati huo huo, Rais Samia alimhamisha Frederick Dagamiko kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Songea kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Aidha, alimhamisha Bashir Muhoja kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea.

Aidha, Rais Samia, alimhamisha, Tito Philemon Mganwa kutoka Halmashauri ya Mji wa Korogwe kwenda kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Wateule hao wameapishwa leo.