April 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Profesa Ibrahim Lipumba, akiwa kwenye mkutano wake wa kampeni

Lipumba aahidi makubwa Dodoma akishika urais 2020

Na Hadija Bagasha Dodoma,

CHAMA cha Wananchi CUF kimeahidi kuhakikisha kinaboresha miundombinu ya makao makuu ya nchi jijini Dodoma iwapo kitapata ridhaa ya kuongoza Serikali katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu.

Ahadi hiyo imetolewa na mgombea urais wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba, Akijinadi katika alipokuwa akihutubia mkutano wake wa kampeni wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.

Amesema ili wananchi wa Dodoma waweze kunufaika na kilimo na ufugaji wanahitaji kutafuta masoko kwa njia ya mtandao.

“Nitakapopata ridhaa hiyo nitahakikisha kilimo cha zabibu kinafuata taratibu za kisasa na kufanya wananchi wa Dodoma waondokana na umasikini kupitia zao hilo ambalo kwa nchi nzima linalimwa mkoa huu (Dodoma),” amesema Profesa Lipumba.

Profesa Lipumba akiwa ameambatana na mgombea mwenza, Hamida Abdalah Huweish, aligeukia ufugaji wa mbuzi akisema mifugo hiyo ni biashara nzuri ndani na nje ya nchi, lakini hakuna utaratibu unaowahakikishia wafugaji ufugaji bora.

“Ndugu zangu wenzetu wa Afrika ya Kati wanapenda mbuzi waliopata malisho ya kawaida kwa hiyo ufagaji wa mbuzi unalipa, sio ndani tu hata nje ya nchi,” amesema Profesa Lipumba.

Aidha amesema ili mbuzi waweze kuwa na soko ni lazima wafanyabiashara wajue kufanya biashara kupitia mitandao na kujenga utaratibu wa vijana kujielimisha.

“Ndugu zangu wananchi sera ya CUF ni kuhakikisha inawekeza kwa vijana na kuhakikisha wanapata elimu bora kuanzia shule za awali,shule za msingi na sekondari” alisema Profesa Lipumba.

Akizungumzia kilimo, Profesa Lipumba amesema katika ilani ya chama hicho wamedhamiria kuboresha kilimo ili mkulima wa kawaida aweze kupata chakula cha kutosha.

Amesema zao la uwele, mtama na ulezi lina soko kubwa duniani kwa kuwa nchi nyingine hutumia mazao hayo kwa chakula cha wanyama.

“Mazao haya yana soko kubwa ndani na nje ya nchi kama tutaweka utaratibu mzuri, Wachina wanahitaji tani nyingi za mtama kwa ajili ya kulishia mifugo yao,” amesema.

Sambamba na hayo, Profesa Lipumba alisema Tanzania inahitaji kuweka utaraibu mzuri wa kufanya mtama kuwa zao la biashara ili wananchi waweze kufaidika na zao hilo.

Kuhusu ufugaji ng’ombe, Profesa Lipumba amesema wamekuwa wakifugwa kienyeji badala ya kutumia utaalamu wa kisasa.

“Bado hatujatumia mifugo yetu kuhakikisha tunajitegemea vizuri kwa maziwa, tunahitaji kuboresha ufugaji ili watoe maziwa ya kutosha kwa ajili ya biashara,” amesisitiza.

Profesa Lipumba amesema ipo haja ya kuweka utaratibu wa kulinda mazingira kulingana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

“Chama chetu cha CUF tumejipanga kushirikiana na wananchi kuleta mabadiliko na mambo haya yanawezekana kama mkituchagua,tunahitaji kuwa na uongozi utakaofuata taratibu na katiba,” alisema

Mgombea ubunge jimbo la Chamwino Diana Simba alisema hali ya kiuchumi katika jimbo hilo imekuwa ngumu kutokana na ubovu wa miundombinu hususani ya barabara.

Aidha Profesa Lipumba alisema atahakikisha anaboresha mfumo wa elimu kwa wanafunzi ili wawe wanapewa kompyuta mpakato zitakazo wasaidia kuwaongezea maarifa.