Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judithy Kapinga amesema Serikali kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) imejipanga kuimarisha sekta ya viwanda nchini kwa kuanzisha miradi ya kimkakati ya utafiti, teknolojia na ubunifu katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri Kapinga amesema TIRDO imepanga kuanzisha Kituo cha Taarifa za Viwanda (NIIMS), mfumo wa ubashiri wa teknolojia pamoja na viatamizi kwa wabunifu wa teknolojia ili kuongeza kasi ya maendeleo ya viwanda nchini.
Amesema shirika hilo pia litafanya tafiti za mnyororo wa thamani wa madini adimu kwa ajili ya maendeleo ya viwanda katika mikoa ya Kagera kupitia Wilaya ya Kyerwa, Singida katika Wilaya ya Iramba na Dodoma kupitia Wilaya ya Mpwapwa.
Aidha, Waziri Kapinga amesema TIRDO itaendelea kukamilisha ithibati za maabara pamoja na kuboresha maabara za kemia, makaa ya mawe, nguo na ngozi, nishati pamoja na mafuta na gesi ili kuongeza ubora wa huduma za utafiti na uchunguzi wa viwanda.
Katika hatua nyingine, amesema shirika hilo linatarajia kuanzisha maabara ya nishati na madini mkoani Njombe pamoja na maabara ya upimaji wa majiko ya kupikia kwa lengo la kuimarisha matumizi ya teknolojia safi na salama ya nishati.
Waziri Kapinga amebainisha kuwa TIRDO pia itajenga kiwanda darasa cha vifaa vya kielektroniki vinavyotumia malighafi zinazopatikana nchini sambamba na kujenga mtambo wa biogas asilia wa ubadilishaji taka kuwa gesi ya petroli iliyosindikwa (LPG) katika masoko ya Mabibo, Ilala Boma na Temeke Stereo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wa taasisi za CAMARTEC, Shirika.la Viwanda vidogo (SIDO) na TEMDO, Waziri huyo alisema kwa pamoja zimepanga kuanzisha kiwanda darasa cha kuchakata chikichi mkoani Kigoma, kuwezesha upatikanaji wa masoko na mikopo kwa wajasiriamali 3,000 pamoja na kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wajasiriamali 21,200 nchini.
Amesema hatua hizo zina lengo la kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani, kukuza ajira na kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa kupitia sekta ya viwanda.

More Stories
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi
Twange aeleza kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa Mradi wa Hale