May 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Viwanda kupanua uchumi Kupitia miradi Mkakati

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judithy Kapinga amesema Wizara hiyo imejipanga kuimarisha maendeleo ya sekta ya viwanda nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri Kapinga amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya viwanda kwa lengo la kuongeza ajira, kukuza uchumi wa viwanda na kuvutia wawekezaji zaidi nchini.

Katika Idara ya Maendeleo ya Viwanda, Waziri Kapinga amesema Wizara imepanga kuanzisha na kuendeleza miundombinu ya viwanda, kufanya tafiti katika sekta za vipaumbele pamoja na kukamilisha kanzidata ya viwanda ili kuongeza ufanisi wa sekta hiyo.

Aidha, amesema kupitia Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi kielelezo ikiwemo miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma, Chuma cha Liganga na Mradi wa Magadi Soda Engaruka.

Alitaja miradi mingine kuwa ni pamoja na mradi wa chuma wa Maganga Matitu, makaa ya mawe Katewaka pamoja na kuendelea kulipia leseni za uchimbaji ili kuhakikisha miradi hiyo inaendelea kwa tija.

“Serikali itaendelea kuboresha Kiwanda cha Mashine na Vipuri cha KMTC, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za kibaiolojia katika kiwanda cha TBPL pamoja na kufufua Kiwanda cha Mang’ula kwa kushirikiana na wawekezaji mahiri,” amesema Waziri Kapinga.

Pia amesema Serikali itaendelea kuboresha miundombinu katika kongani za viwanda na kuanzisha kongani kubwa na ya kisasa kwa lengo la kuvutia uwekezaji zaidi wa viwanda nchini.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema Serikali itaendeleza mashamba ya miti ya mpira kwa ajili ya kuzalisha malighafi za viwanda sambamba na kuhifadhi mazingira, huku pia ikitarajia kujenga jengo la ofisi za Shirika hilo jijini Dodoma.

Amesema utekelezaji wa mipango hiyo unalenga kuongeza mchango wa sekta ya viwanda katika pato la taifa na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi wa nchi.