Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, ameliomba Bunge kuidhinisha jumla ya shilingi bilioni 137.8 huku akitaja vipaumbele saba vitakavyotekelezwa katika mwaka wa fedha 2026_2027.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri Kapinga amesema kati ya fedha hizo, shilingi 104,122,530,000 ni kwa matumizi ya kawaida huku shilingi 33,690,103,000 zikitengwa kwa matumizi ya maendeleo.
Amefafanua kuwa kati ya fedha za matumizi ya kawaida, shilingi 78,049,345,000 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na shilingi 26,073,185,000 ni matumizi mengineyo. Aidha, alisema fedha zote za maendeleo zitakuwa ni za ndani.
Waziri Kapinga amesema mpango na bajeti ya Wizara kwa mwaka 2026/2027 umezingatia miongozo mbalimbali ya taifa ikiwemo Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano wa 2026/2027 hadi 2030/2031, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 pamoja na sera, sheria na maelekezo mbalimbali ya Serikali.
Pia amesema bajeti hiyo imezingatia Mpango Mkakati wa Wizara wa mwaka 2026/2027 hadi 2030/2031, maoni ya Kamati za Kudumu za Bunge na maagizo ya viongozi wakuu wa Serikali.
Akieleza maeneo ya vipaumbele kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Waziri Kapinga amesema Wizara itaendelea kutekeleza miradi ya kimkakati na ya kielelezo ya viwanda sambamba na kuimarisha uwezo wa uzalishaji viwandani kupitia kuboresha mazingira wezeshi ya biashara.
Amesema Serikali pia itaendelea na ujenzi wa miundombinu ya kongani za viwanda na mitaa ya viwanda kwa ajili ya kusaidia viwanda vidogo na vya kati ili kuongeza uzalishaji na ajira.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Wizara itaendelea kuchochea maendeleo ya viwanda na biashara kupitia ubunifu, matumizi ya teknolojia za kisasa, elimu pamoja na mafunzo ya ujuzi kwa vijana na wajasiriamali.
Ameongeza kuwa juhudi pia zitaelekezwa katika kuimarisha upatikanaji wa fedha na mitaji kwa wajasiriamali na wazalishaji viwandani, kuboresha mazingira ya biashara na kukuza sekta binafsi.
Katika hatua nyingine, Waziri Kapinga amesema Wizara itaendelea kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika soko la ndani na nje ya nchi.
Aidha, amesema Serikali imepanga kuanzisha na kuendeleza vituo vya ubunifu na biashara kwa vijana kwa lengo la kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.

More Stories
Itunda: Serikali yaleta mageuzi hospitalini
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi