Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judithy Kapinga, amesema Serikali imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya “Lumbesa” ili kulinda haki za wakulima, wafanyabiashara na wanunuzi wa mazao nchini.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni, Waziri Kapinga amesema Wizara kupitia Wakala wa Vipimo (WMA) imeendelea kusimamia matumizi sahihi ya vipimo katika biashara na uchumi kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340.
Amesema Serikali imebaini kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ufungashaji na uuzaji wa mazao kinyume na sheria hiyo, maarufu kama “Lumbesa”, ambapo baadhi ya wafanyabiashara huzidisha uzito unaoruhusiwa katika magunia ya mazao.
“Sheria inaelekeza mazao yaliyofungashwa kwa namba, idadi au uzito kutopaswa kuzidi kilogramu 100 pamoja na kiwango himilivu cha asilimia tano,” amesema Waziri Kapinga.
Aidha, amesema sheria pia inawataka wauzaji na wanunuzi kutumia mizani inayohakikiwa na Wakala wa Vipimo angalau mara moja kwa mwaka.
Katika kukabiliana na changamoto hiyo, Waziri Kapinga alisema Wizara imeendesha operesheni tisa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Pwani, Morogoro, Mbeya, Iringa na Njombe.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, magari 2,500 yaliyokuwa yakisafirisha mazao yalikaguliwa, huku magari 81 yakibainika kukiuka sheria kwa kusafirisha mazao yaliyofungashwa kinyume na viwango vinavyokubalika.
Amesema hatua mbalimbali zilichukuliwa dhidi ya wahusika, ikiwemo kutozwa faini za papo kwa papo pamoja na kuamriwa kufungasha upya mizigo yao kwa kuzingatia sheria.
Waziri Kapinga alibainisha kuwa operesheni hizo zinaendelea nchini kote kupitia ofisi za mikoa za Wakala wa Vipimo, kwa lengo la kutokomeza kabisa tatizo la Lumbesa.
Pia amesema Serikali imeboresha huduma za uhakiki wa vipimo kwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia vituo vya muda 5,050 vilivyowekwa katika maeneo ya kata, mitaa na vijiji.
Aidha, baadhi ya halmashauri zikiwemo Mpanda, Kasulu na Kibondo zimeanzisha sheria ndogo zinazosisitiza matumizi ya mizani iliyohakikiwa katika biashara ya mazao.

More Stories
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi
Twange aeleza kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa Mradi wa Hale