Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), hatua inayolenga kuongeza ubora wa elimu na kukidhi ongezeko la wanafunzi nchini.
Akisoma bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri Kapinga amesema kupitia CBE, Serikali inaendelea na ujenzi wa jengo la ghorofa 10 la Metrology Complex katika kampasi ya Dar es Salaam.
Amesema hadi kufikia Aprili 2026, ujenzi wa jengo hilo ulikuwa umefikia asilimia 93, huku kiasi cha shilingi bilioni 8.88 kati ya bilioni 10.39 zilizotengwa kwa hatua ya kwanza tayari zikiwa zimetumika.
“Jengo hilo litakapokamilika litakuwa na jumla ya kumbi 29 za mihadhara zenye uwezo wa kubeba wanafunzi 4,160 kwa wakati mmoja, jambo litakaloboreshwa mazingira ya kufundishia na kujifunzia,” amesema Waziri Kapinga.
Ameeleza kuwa maboresho ya miundombinu yanaenda sambamba na uboreshaji wa mitaala na programu za mafunzo ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira pamoja na maendeleo ya teknolojia.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, CBE imeendelea kusisitiza elimu ya vitendo kupitia Programu ya Uanagenzi inayowapa wanafunzi nafasi ya kutumia nusu ya muda darasani na nusu nyingine maeneo ya kazi kwa ajili ya kupata uzoefu halisi.
Aidha, amesema hadi Aprili 2026, mitaala mipya minane ilikuwa imeidhinishwa na kufanya jumla ya mitaala iliyopitishwa kufikia 71, huku mitaala mingine 28 ikiwa katika hatua mbalimbali za maandalizi na uthibitishaji.
Waziri Kapinga amesema kuongezeka kwa mitaala hiyo kumechangia ongezeko la udahili wa wanafunzi katika chuo hicho, ambapo idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 20,029 mwaka wa masomo 2023/2024 hadi kufikia wanafunzi 24,957 mwaka wa masomo 2025/2026.
Amebainisha kuwa ongezeko hilo la wanafunzi linaifanya Serikali kuendelea kuwekeza katika miundombinu bora na ya kisasa ili kuhakikisha mazingira ya kujifunzia yanakuwa rafiki na yenye tija kwa maendeleo ya elimu nchini.

More Stories
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi
Twange aeleza kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa Mradi wa Hale