Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO) imeendelea kuimarisha bunifu za wajasiriamali kupitia programu atamizi zinazolenga kukuza uzalishaji wa viwandani na kuongeza ajira nchini.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027 bungeni jijini Dodoma, Waziri Kapinga amesema TEMDO imeendelea kuwasaidia wajasiriamali wabunifu kwa kuwawezesha kupata huduma mbalimbali ikiwemo maeneo ya kufanyia kazi, mashine na mitambo, ushauri wa kiufundi pamoja na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili waweze kukua na kufikia viwango vya kujitegemea.
Ameeleza kuwa hadi kufikia Aprili 2026, jumla ya wajasiriamali wabunifu watano ambao ni Bivac Co. Ltd, Rest Food Process Ltd, Upendo Food Process Ltd, Simba and Alice Food Process Ltd pamoja na Neema Nafaka Products wameendelea kuzalisha bidhaa zitokanazo na mazao ya kilimo kupitia kiatamizi cha TEMDO kilichopo Mkoa wa Arusha.
Waziri Kapinga amesema kupitia programu hiyo, jumla ya ajira 220 zimezalishwa ambapo ajira 100 ni za moja kwa moja huku ajira 120 zikiwa zisizo za moja kwa moja.
Ametaja baadhi ya bidhaa zinazozalishwa kupitia kiatamizi hicho kuwa ni pamoja na siagi ya karanga, unga lishe, vyakula vya lishe, biskuti pamoja na virutubisho mbalimbali vinavyotokana na mazao ya kilimo.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya ubunifu wa viwanda nchini kwa kuweka mifumo rafiki itakayowawezesha wabunifu na wajasiriamali wadogo kukua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya sekta ya viwanda nchini.

More Stories
MNEC Mwaselela: CCM kimechagua siasa za maendeleo
TMA yatoa elimu ya hali ya hewa kwa wavuvi
Twange aeleza kutoridhishwa na kasi ya Mkandarasi wa Mradi wa Hale