May 22, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TAKUKURU ya okoa mil.624.6

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Kagera

TAASISI ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkoa wa Kagera imesaidia kurejesha kiasi cha sh.milioni 624.6 baada ya kushinda mashauri 50 kati ya 52 yaliyofikishwa katika mahakama mbalimbali mkoani humo.

Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kagera, Leonard Swai ametoa taarifa hiyo Mei 21 mwaka huu,ofisini kwake wakati akizungumza na waandishi wa habari,amesema kuanzia Julai ,2025 hadi sasa imefanikiwa kufungua kesi 61 mahakamani,ambapo mashauri 52 yameamuliwa kati ya hayo taasisi hiyo imeshinda mashauri 50 sawa na asilimia 97,imeshindwa mashauri mawili huku mashauri 9 yanaendelea mahakamani.

Amesema katika mashauri hayo 50 waliyoshinda wamefanikiwa kurejesha kiasi cha zaidi ya sh.milioni 624.6.

Hata hivyo amesema kipindi cha Januari hadi Machi 2026,wamepokea taarifa 132 kati ya hizo 83 zilihusu rushwa na zilichunguzwa ambapo jumla ya majalada 12 yalifunguliwa kesi mahakamani na chunguzi zingine zinaendelea huku taarifa 49 hazikuhusu rushwa.

Ameongeza kuwa TAKUKURU Wilaya ya Kyerwa imesaidia kurejesha fedha kiasi cha sh. milioni 30, zilizotolewa kwa ajili ya mkopo wa kikundi cha ufugaji nyuki cha wanawake wa Kata ya Katera ambazo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri inayotolewa kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema kikundi hicho kilipokea fedha kupitia akaunti ya kikundi namba 35910010751 iliyopo benki ya NMB Februari 18 mwaka huu baada ya kuonekana kutimiza masharti yote ya mkopo.

Amesema baada ya uchunguzi wa TAKUKURU ilibaini kuwa kikundi hicho kimetumika kama kikundi kivuli cha kupata mkopo husika wa milioni 30,baada ya kikundi hicho kuwekewa fedha hizo zilihamishiwa kwenye akaunti namba 01J2033984900 inayomilikiwa na Benjamin Barthazary ambaye alizitumia fedha hizo kwa matumizi yake binafsi.

Ameeleza kuwa, baada ya kubaini kasoro hizo TAKUKURU Kyerwa ilielekeza fedha hizo zirejeshwe kwenye Halmashauri ya Kyerwa ili zitumike kwenye makundi yenye sifa na tayari zimesharejeshwa kwenye akaunti ya halmashauri.

Wakati huohuo, wamefanikiwa kudhibiti ujenzi wa chini ya kiwango msingi wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Runzenze Kata Ntobeye wilayani Ngara inayojengwa kwa nguvu za wananchi na jumla ya sh.milioni 9.5 kimekusanywa na wananchi wa kijiji hicho kwa ajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.

Amesema ufuatiliaji huo ulibaini kuwa kiwango cha uwiano katika mchanganyiko wa zege katika jamvi la msingi huo kuwa ni dhaifu kiasi cha kusababisha kuanza kumomonyoka na nondo zilizosukwa kuonekana na kuanza kupata kutu hali inayoashiria ujenzi umefanyika chini ya kiwango.

Hata hivyo taasisi hiyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, waliishauri Serikali ya Kijiji kufanya marekebisho katika hatua hiyo ya ujenzi ili kuzuia madhara ambayo yangejitokeza kutokana na udhaifu wa msingi huo jambo ambalo limekwisha tekelezwa.