June 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mtanda asisitiza matumizi ya takwimu serikalini

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza

MAOFISA Mawasiliano wa Serikali hapa nchini wametakiwa kuachana na utoaji wa taarifa kwa kutumia hisia na badala yake wajenge utamaduni wa kutoa taarifa zenye ushahidi,takwimu sahihi na mifano halisi ili kujenga imani kwa wananchi.

Hayo yameelezwa Juni 2,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Said Mtanda,wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Maofisa Mawasiliano(TAGCO), na kongamano la wanamawasiliano wa Serikali,unaofanyika jijini Mwanza kwa siku tano kuanzia Juni 1-5,2026.

Ambapo amewataka wataalamu wa mawasiliano kuisaidia Serikali kwa kutoa taarifa zenye ushahidi kwa kuhakikisha wanaonesha wananchi wangapi wamefikiwa na huduma fulani, maisha ya wananchi kadhaa yameboreshwa kutokana na mpango fulani au ajira zipi zimezalishwa kutokana na utekelezaji wa mradi fulani.

“Serikali inayotumia taarifa na takwimu sahihi na mifano halisi inajenga imani kwa wananchi,tusiwasiliane kwa hisia pekee wala kwa kauli za jumla bali tuwasiliane kwa ushahidi,”amesema Mtanda na kuongeza:

“Pia muwe na uwezo wa kutafsiri takwimu hizo kwa lugha rahisi, mwananchi hahitaji kusikia namba nyingi zisizo na maana kwake bali anahitaji kuelewa taarifa hizo zinagusa vipi maisha yake,”.

Mtanda pia amewahimiza kujenga uhusiano wa karibu na wataalamu wa takwimu, mipango, ufuatiliaji na tathmini ndani ya taasisi zao, kwa sababu mawasiliano yenye nguvu ni yale yanayounganisha ukweli, ushahidi, lugha rahisi, takwimu na matumizi sahihi ya njia za kufikisha ujumbe.

Mkurugenzi wa Takwimu za uchumi kutoka ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS), Daniel Masolwa,amesema takwimu ni mali ya umma na zinapaswa kutumiwa kwa uwazi bila kufichwa ili kuwanufaisha wananchi.

“Wanahabari na Maofisa Mawasiliano wanapaswa kutumika kama kiungo muhimu kufikisha takwimu kwa wananchi. Takwimu zikitafsiriwa vizuri huongeza uelewa wa umma kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo,” amesema Masolwa.

Masolwa amesema matumizi ya data katika uandishi wa habari yanaongeza ubora wa taarifa kwa kuwa takwimu husaidia kuthibitisha hoja na kufanya habari ziwe na nguvu zaidi.

Ofisa Habari wa Kampuni ya Uendelezaji Joto ardhi Tanzania (TGDC), Boaz Mazigo,amesema takwimu ni nyenzo muhimu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali kwa kuwa zinatoa picha halisi ya mazingira na kusaidia viongozi pamoja na taasisi kufanya maamuzi yenye tija.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TAGCO Karimu Meshack,amesema kwa sasa chama hicho kina wanachama zaidi ya 650, lakini wapo wataalamu wa mawasiliano wasio punguza 500 bado hawajajiunga na chama hicho.

Meshack amesema,TAGCO imefanikiwa kuanzisha mifumo ya kidigitali,ambayo imeongeza uwazi,uwajibikaji,ufanisi na kuimarisha huduma kwa wananchama na viongozi pamoja na kununua kiwanja kwa ajili ya kujenga makao makuu ya ofisi ya chama hicho.