Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI imesema itaendelea kuimarisha mazingira ya wafanyabiashara wadogo kwa kujenga masoko ya machinga na miundombinu wezeshi ili kuongeza fursa za ajira na kukuza uchumi wa vijana nchini.
Akizungumza na Waandishi wa habari katika Soko la Machinga Barabara ya Bahi jijini Dodoma,leo Julai 22,2026 Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo,Gerson Msigwa alipofanya ziara na kuzungumza na baadhi ya wafanyabiashara ambapo ambapo amesema soko hilo lilijengwa mwaka 2022 kwa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na lilikuwa na uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara 2,700, lakini kwa sasa linahudumia zaidi ya machinga 4,800, wengi wao wakiwa vijana.

Amesema Soko hilo ni sehemu ya masoko 15 ya machinga yanayojengwa nchini, ambapo masoko 10 yamekamilika kwa asilimia 100 na mengine matano yako katika hatua mbalimbali za ukamilishaji. Serikali imetumia zaidi ya shilingi bilioni 15 kutekeleza mradi huo.
Aidha,amesema Halmashauri mbalimbali zimeendelea kujenga masoko mengine madogo ya machinga yenye uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara kati ya 500 na 1,500, hatua inayolenga kupanua nafasi za biashara na kupunguza msongamano katika masoko yaliyopo.
Msigwa amesema kuwa soko la Machinga la Dodoma hupokea zaidi ya wanunuzi 10,000 kwa siku, huku likiwa soko la bidhaa mbalimbali kutoka maeneo tofauti ya nchi, jambo linalowanufaisha pia wakulima na wazalishaji wa ndani kwa kupata soko la uhakika.

Alibainisha kuwa serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo, ambapo bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huu imezidi shilingi trilioni 1.1 ili kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kuhakikisha bidhaa zinawafikia wananchi zikiwa na ubora unaohitajika.
Pia amesesisitiza kuwa masoko hayo yamekuwa fursa kwa wazalishaji wa bidhaa zinazoongezwa thamani nchini, ikiwemo mafuta ya kula yanayotengenezwa na viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vya Watanzania, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani.
Akihitimisha, aliwataka vijana kutumia fursa zilizowekwa na serikali kwa kujihusisha na biashara na shughuli nyingine za uzalishaji badala ya kupoteza muda katika shughuli zisizo na tija, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuongeza maeneo ya biashara ili kuwainua kiuchumi wananchi, hususan vijana.


More Stories
Mwanasheria Mkuu afungua mkutano wa Mwaka wa TIArb
Kituo cha afya Ibungilo chafikia asilimia 25
Sangu: Viongozi washirikiane bila kujali vyama vyao