September 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Jalsa Salana ya 55 kukutanisha washiriki 5,500

Na Mwandishi wetu,TimesMajira

ZAIDI ya washiriki 5,500 kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuhudhuria Mkutano wa Mwaka (Jalsa Salana) wa 55, unaolenga kuwaimarisha waumini kiroho kwa kuongeza hofu ya Mwenyezi Mungu, uchamungu, huruma na upendo, huku wakijiepusha na mambo mabaya.

Mkutano huo umeandaliwa na Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania na utakuwa na kaulimbiu isemayo, “Taqwa (Uchamungu) Ndiyo Msingi wa Kila Wema.”

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Septemba 22, 2026, Amiri na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya hiyo, Sheikh Khawaja Muzaffar Ahmad, amesema Jalsa hiyo itafanyika Septemba 25 hadi 27, mwaka huu, katika eneo la Kitonga, Kata ya Msongola, Manispaa ya Ilala, jijini Dar es Salaam.

Amesema mkutano huo pia utajadili changamoto zinazoikabili dunia, ikiwemo migogoro na vita, huku waumini wakipata fursa ya kushiriki ibada, mihadhara na mafundisho ya dini, pamoja na Sala ya usiku (Tahajjud).

Aidha, amesema waumini wamehimizwa kushiriki shughuli za kijamii, ikiwemo kuwasaidia wenye mahitaji na kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa, huku akieleza kuwa Jumuiya hiyo ina uwepo katika nchi 212 duniani.

Kwa upande wake, Naibu Amir wa Ahmadiyya Muslim Jamaat Tanzania, Abdurahman Mohamed Ame, amesema maadili ni msingi muhimu wa maisha ya mwanadamu na kwamba Uislamu unasisitiza kuishi kwa maadili mema katika kila hatua ya maisha.

Amesema mafundisho ya Uislamu yanamtaka mtu kusema ukweli, kuheshimu haki za wengine na kutambua kuwa katika kudai haki zake, anapaswa pia kutekeleza wajibu wake bila kuvunja haki za wengine.

“Ni kweli kudai haki zetu, lakini tukumbuke wajibu wetu na tuhakikishe kwamba wakati tunadai haki, tusije tukateleza, tukavunja haki au wajibu wetu, au tukavunja haki za wengine kwa kisingizio cha kudai haki zetu,” amesema.

Ameongeza kuwa maadili mema katika familia na jamii ni msingi wa amani, akisema dunia ikiheshimu haki za wengine na kuzingatia maadili, migogoro na matatizo yanaweza kupungua.