July 23, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maboresho sheria yaongeza ushiriki wa watanzania kwenye migodi

*Mavunde awataka watanzania kuunganisha nguvu na kutoa huduma bora

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online- Mwanza 

WAZIRI  wa Madini Anthony Mavunde  amesema Serikali imeendelea  kushuhudia ongezeko la ushiriki wa Watanzania katika utoaji wa huduma na usambazaji wa bidhaa kwenye migodi tangu kufanyika kwa maboresho ya Sheria ya Madini na kanuni zake.

Huku akiwataka watoa huduma katika migodi hapa nchini kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa pamoja ili kuchangamkia fursa zinazoongezeka katika sekta hiyo hususani katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma bora zinazokidhi viwango vinavyohitajika.

Mavunde amezungumza hayo Julai 22,2026,wakati akizindua jukwaa la tano la utekelezaji wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini,linalofanyika mkoani Mwanza na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta hiyo ambapo alisema,Serikali inatarajia kuona asilimia 90 ya bidhaa na huduma zinazotumika katika migodi zikizalishwa na kutolewa na Watanzania. 

Amesema ununuzi wa bidhaa na huduma katika sekta ya madini umefikia kiasi cha sh.trilioni 5.1 kwa mwaka, hali inayoonesha ukubwa wa fursa zilizopo kwa wazalishaji na watoa huduma wa ndani huku sekta  hiyo imezalisha ajira rasmi 20,421, ambapo ajira 16,695 zinashikiliwa na watanzania huku mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa umeendelea kuongezeka na kufikia asilimia 10.1.

“Mpaka sasa tumeshuhudia watendaji wakuu na mameneja wa migodi wakiwa watanzania.Haya ni mafanikio tofauti na zamani, ambapo nafasi nyingi za uongozi katika migodi ya madini zilishikiliwa na raia wa kigeni,”amesema Mavunde.

Pia amesema,mafanikio mengine ni kuanzishwa kwa masoko ya madini 44 na vituo vya ununuzi wa madini 117, hatua ambayo imechangia kuongeza ukusanyaji wa maduhuli yatokanayo na sekta hiyo  kutoka sh.bilioni 161  mwaka wa fedha 2015/2016 hadi sh.trilioni 1.393 katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Sanjari na hayo Mavunde amesema, ongezeko la uwekezaji katika sekta ya madini na matarajio ya kuanzishwa kwa migodi mipya linatarajiwa kufungua fursa zaidi kwa watanzania,hivyo watoa huduma wanapaswa kujiandaa kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani, kuongeza ubora wa bidhaa,huduma na kujenga uwezo wa kushindana katika soko.

Hata hivyo amesema utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, ya kuanzisha hifadhi ya dhahabu katika Benki Kuu ya Tanzania, ulioanza rasmi Oktoba 1, 2024, umeiwezesha Tanzania kuwa na hifadhi ya dhahabu yenye uzito wa tani 28 na kuiweka nchi miongoni mwa mataifa matano barani Afrika yenye hifadhi kubwa ya dhahabu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini,Mhandisi Yahya Samamba,amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya madini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.

Mhandisi Samamba amewataka watoa huduma katika migodi kutoa huduma bora kwa kuzingatia weledi,uadilifu na viwango vinavyokubalika, akisisitiza kuwa wizara itaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali na kufanya kazi kwa karibu zaidi na wadau wa sekta ya madini.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema,juhudi zinazofanywa na Wizara ya Madini za  kuendelea kuvutia uwekezaji katika Mkoa wa Mwanza umechangia kuanzishwa kwa mgodi wa dhahabu wa Sotta Mining, ambao unatarajiwa kutoa ajira 1,500 utakapoanza uzalishaji.

Naye Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Dkt.Janet Lekashingo amesema,jukwaa la hilo  limekuwa na manufaa  katika kuchochea ushiriki wa watanzania katika sekta hiyo ambayo yanaonekana  kupitia ongezeko la uwasilishaji wa mipango ya ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini, kutoka mipango 51 mwaka 2018 hadi kufikia mipango 1,312 mwaka 2025.