Na.Mwandishi wetu,Timesmajira
Wizara ya Afya, Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi imekutana na wataalam mbalimbali wanaotoa huduma za Afya Ngazi za Jamii Wilayani Bukombe Mkoani Geita kwa lengo la kuwajengea uwezo kuhusu utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi Jamii.
Mkuu wa Wilaya ya Bukombe Paskasi Muragili amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ni muhimu sana katika kutoa Elimu ya Afya kwa jamii kwani Wilaya ya Bukombe bado inakabiliwa na changamoto ya malaria,lishe pamoja na changamoto za Afya ya Mama na Mtoto.
Kiongozi huyo amebainisha hayo leo tarehe 22 Julai, 2026 Wilayani Bukombe Mkoani Geita wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi hicho kilichowakutanisha kamati tendaji za kata, baadhi ya watoa huduma za afya ngazi ya jamii na Waganga wafaidhi wa Vituo vya Afya.
Muragili ameangazia umuhimu wa huduma inayotolewa na Muhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuliko mchakato wa upatikanaji wake akiangazia namna ambavyo serikali ya sasa ilivyowekeza katika kuokoa maisha ya mama na mtoto.

‘’Kama mtoa huduma za Jamii atatoa Elimu ya Afya mapema na mama akaanza mapema huduma za kliniki tutapunguza kwa kabisa vifo vya mama na mtoto, ikiwemo malaria na afua mbalimbali za lishe,’’ameongeza Kiongozi huyo.
Naye Afisa Mpango wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya Bahati Mwailafu amesema Wahudumu hao wanapatiwa elimu ya utekelezaji wa Mpango huo akiitaja Bukombe kuwa eneo la Mfano kati ya Halmashauri zinazotekeleza Mpango huo kuanza kupima na kutoa dawa kwa wagonjwa wa malaria.m

‘’Bukombe ni Halmashauri ya mfano iliyochaguliwa kwenye Halmashauri 184 nchini inayojengewa uwezo wa kupima malaria katika kaya na kutoa dawa’’, ameongeza Mwailafu.
Akiwasilisha mada yake kwa wajumbe wa Kikao kazi hicho Afisa Mpango wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya Orsolina Tolage amesema Muhudumu wa Ngazi ya Jamii anawajibika kushiriki katika vikao vya Kijiji na kupewa fursa ya kutoa Mawazo kuhusiana na huduma za kiafya zinazotolewa katika Kituo husika.
Muhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwa mujibu wa Mwongozo anafanya kazi katika yale maeneo ya Jamii ambayo yako katika mazingira ambayo hayana vituo vya Afya na taarifa zao kutumiwa na wataalam wa Afya kufanyia kazi changamoto zilizoibuliwa na muhudumu husika.

More Stories
Maboresho sheria yaongeza ushiriki wa watanzania kwenye migodi
Prof.Kabudi:Tumepiga hatua utoaji huduma za Afya
Masoko ya machinga kufungua fursa kwa vijana nchini