June 2, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Milioni 299 kutumika kujenga ofisi za kata

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online- Mwanza

HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,inatarajia kutumia kiasi cha sh.milioni 299, kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mbili za Kata ya Buswelu na Kawekamo.

Hiyo ni baada ya Halmshauri hiyo kusaini mkataba na INTERGO Company Ltd kwa ajili ya ujenzi wa ofisi mbili za Kata ya Buswelu na Kawekamo,ambapo hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha sh.milioni 299 pamoja na VAT.

Ikumbukwe kuwa wananchi wa maeneo hayo walijikuta katika hadha ya kutokuwa na ofisi ya kata kwa takribani miezi saba,baada ya majengo ya ofisi za Kata za Buswelu na Kawekamo,kuwa miongoni mwa mali za umma zilizochomwa moto na kuharibiwa wakati wa vurugu zilizotokea kipindi cha uchaguzi mkuu Oktoba 29,2025.

Akizungumza jana wakati wa zoezi hilo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Sarah Ng’hwani, amesema ujenzi wa ofisi hizo za kata zinatarajiwa kujengwa kwa muda wa siku 90 sawa na miezi mitatu.

Hivyo amemtaka mkandarasi wa ujenzi wa ofisi hizo INTERGO CO.LTD kuhakikisha wanaitekeleza kazi hiyo kwa ubora wa hali ya juu huku wakizingatia muda wa mkataba huo.

Hiyo yote ni jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali katika kuhakikisha wanarejesha miundombinu ilioharibiwa kipindi cha vurugu hizo.