April 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Majaliwa kuwatunuku vyeti wanafunzi waliosoma nje

Na Holiness Ulomi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mahafali yapili ya kimataifa kwa wanafunzi waliosoma nje ya nchi yanayotarajiwa kufanyika mwishoni mwa wiki hii Mlimani City, jijini Dar es Salaam.

Mahafali hayo yanayotarajiwa kuwakutanisha wanafunzi 400 waliosoma vyuo vikuu mbalimbali nje ya nchi kupitia taasisi ya elimu nje ya nchi ya Global Education Link (GEL).

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa (GEL), inayowaunganisha wanafunzi na vyuo vikuu nje ya nchi, Abdulmalik Mollel, wakati akizungumza kwenye kikao cha maandalizi ya mahafali hayo.

Alisema lengo la mahafali hayo ni kuhakikisha wanafunzi Watanzania waliosoma nje ya nchi hawarudi kimya kimya na kinyonge, kwani wao ni wazalendo walioamua kuacha fursa zilizoko huko baada ya masomo yao na kuja kuijenga nchi yao.

Mollel alisema wahitimu hao waliaminiwa na taifa na ndiyo sababu walipewa viza za kwenda kusoma nje ya nchi kwa ajili ya manufaa yao familia zao na kwa ajili ya nchi yao hivyo kurudi kwao ni kurejesha furaha nyumbani, kwani wanatarajiwa kutoa mchango mkubwa kwa nchi.

Alisema GEL itawakutanisha wanafunzi hao kwa ajili ya kujenga mtandao na taasisi na watu mbalimbali hapa nchini baada ya kukaa nje ya nchi kwa muda mrefu ambako huko walishajenga aina nyingine ya maisha.

“Mfano mtoto ameenda huko akiwa na miaka 17 amekaa huko miaka minne au sita anarudi amekuwa mtu mzima amekuta mambo mapya sasa akifika akikosa timu kama aliyokuwa nayo kule anakata tamaa sasa kitendo cha kumkutanisha mtu aliyekuwa Uingereza, India, China, Canada au Afrika kusini kwenye jengo moja ni jambo kubwa sana na la msingi,” alisema Mollel

Aidha, Mollel alisema wanafunzi hao wakikutanishwa wataona kama milango ya maisha yao imefunguliwa kwani watatengeneza mtandao mpya na wenzao waliomaliza nao mwaka mmoja kwenye vyuo hivyo nje ya nchi kwasaab awali hakukuwa na mahafali ya aina hiyo.

Kwa mujibu wa Mollel, mahafali hayo ni fursa kwa wahitimu hao kwani kuna makampuni mbalimbali ambayo yametoka kwenye nchi mbalimbali ambazo wanafunzi hao walisoma ambazo zitakuwa zinatafuta wataalamu wa fani wanazozihitaji hivyo wakikutanishwa itakuwa na manufaa kwao.

“Kuna wawekezaji ambao wanatafuta watu waliosoma kwenye nchi zao angalau wenye kujua lugha zao kidogo sasa hii ni nafasi ya kuwaita hawa kwamba nani amewekeza nini na anahitaji vijana wataalamu sasa ukiwakutanisha ni fursa kubwa sana kwa wawekezaji na vijana,” alisema Mollel

Alisema kuna taasisi za Serikali kama menejimenti ya utumishi wa umma na ile ya kutafutia watu ajira ya TAESA wanahitaji rasilimali watu ambazo zipo lakini hakuna daraja lililowakutanisha hivyo mahafali hayo ni daraja la kuwaunganisha wahitimu hao na taasisi hizo.

Alisema taasisi hizo za Serikali na za binafsi zitakaposhiriki kwenye mahafali hayo zitapata kujua orodha ya wanafunzi waliosoma fani mbalimbali wanazohitaji hivyo kutengeneza daraja baina ya pande hizo mbili na kuondoa malalamiko kwamba kuna uhaba wa wataalamu na vijana kulalamikia tatizo la ajira .